WAKULIMA wa michikichi mkoani Kigoma wameanza kupanda aina mpya ya miche ya tenera yenye kutoa mafuta mengi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye wakati alipofanya mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya jana.
Katibu Mkuu yupo Kigoma kwa ziara ya kikazi kukagua utekelezaji wa agizo la serikali la kuongeza uzalishaji michikichi nchini.
“Zao la chikichi ndio lenye upekee wa kuwafanya wakulima wa Kigoma kuwa na uchumi imara na uhakika wa kipato kutokana na malighafi hiyo ya kuzalisha mafuta ya kula kuhitajika nchini kwa wingi,” alisema Andengenye.
Kutokana na wakulima kuhamasika Mkuu huyo wa Mkoa wa Kigoma aliomba Wizara ya Kilimo kupitia Kituo cha Utafiti wa zao la chikichi (TARI) Kihinga na Wakala wa Mbegu (ASA) kuongeza kasi ya kuzalisha aina hiyo bora ya miche ya chikichi.
“Halmashauri zetu zimejipanga kutekeleza agizo la serikali la kuongeza uzalishaji chikichi na mazao mengine ya biashara ikiwemo korosho ili wakulima wetu wawe na uhakika wa kipato hivyo wizara itusaidie kupata miche na mbegu bora na ziwafikie wakulima kwa gharama nafuu,” alisisitiza Andengenye.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya alisema Wizara inaendelea kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la kuhakikisha zao la chikichi linalimwa kote nchini ambapo hali ya hewa inafaa ili nchi ikabiliane na tatizo la upungufu wa mafuta ya kula.
Kusaya alibainisha mikakati ya wizara kuwa vituo vya utafiti vya TARI Kihinga na shamba la mbegu la ASA Bugaga vilivyopo Kigoma vitaendelea kuzalisha mbegu bora na miche ya michikichi na kuigawa kwa wakulima kwa gharama nafuu.
Katibu Mkuu huyo wa kilimo alitoa wito kwa uongozi wa mkoa wa Kigoma kuhamasisha halmashauri zake kupanda walau miche bora 100,000 ya michikichi bora ili mkoa huo ulio na hali nzuri ya hewa iongeze uzalishaji.
Wizara ya Kilimo inaendelea na jitihada za kuzalisha miche mingi zaidi na kuisambaza kwenye mikoa 17 nchini ambapo zao la michikichi linastawi vyema.