Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kigoma wakamilisha madarasa ya fedha za Covid-19

A3eb7969ba6fa1bd8c95bcfbfec693f4.png Kigoma wakamilisha madarasa ya fedha za Covid-19

Sat, 1 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali mkoani Kigoma imesema kuwa imekamilisha mpango wa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari na shule shikizi unaotekelezwa kwa mkopo wa Benki ya Dunia kupitia mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya Covid-19.

Mkuu wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye akitoa taarifa mwishoni mwa ziara ya kutembelea na kukagua ujenzi wa madarasa hayo katika wilaya za Mkoa Kigoma, alisema mpango wa ujenzi wa madarasa hayo umefanikiwa na lengo la kuhakikisha wanafunzi wanavitumia vyumba hivyo vya madarasa shule zikifunguliwa Januari 17, mwaka huu litatimia.

Andengenye alisema kuwa Mkoa wa Kigoma umepangiwa jumla ya madarasa 638 yatakayogharimu kiasi cha Sh bilioni 15 ambapo kati ya madarasa hayo 550 yatajengwa kwenye shule za sekondari na vyumba vya madarasa 86 vitajengwa katika shule shikizi huku mkoa ukipangiwa kujengwa mabweni mawili kwenye shule za watoto wenye mahitaji maalumu.

Mkuu huyo wa mkoa akiongoza kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na maofisa kutoka idara ya elimu ya sekretatieti ya mkoa Kigoma alisema kuwa karibu wilaya zote zimekamilisha ujenzi wa madarasa hayo na kwamba Wilaya ya Uvinza ndiyo pekee ambayo inakabiliwa na changamoto ya ukamilishaji wa baadhi ya madarasa.

Alisema kuwa hali hiyo inatokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kuchelewa kutolewa kwa fedha kwa shule shikizi kutokana na uhakiki uliofanywa na Tamisemi na changamoto ya ubovu wa barabara katika baadhi ya maeneo kutokana na mvua nyingi hivyo kazi ya kupeleka vifaa maeneo ya ujenzi kuwa ngumu na kuchelewa.

Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Simon Hanange alisema kuwa kuwepo kwa akiba ya matofali kwenye shule za wilaya hiyo na kujiandaa na ujenzi wa vyumba vya madarasa hata kabla ya kuja kwa mradi huo kumeleta mafanikio kumaliza ujenzi wa madarasa yao kwa wakati.

Hanange alisema kuwa pamoja na changamoto ya mvua, kupanda kwa gharama za vifaa vya ujenzi na wazabuni wa vifaa kama madawati na madirisha ya alminium kuwa na kazi nyingi wamepambana kuhakikisha changamoto hizo hazikwamishi malengo yao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live