Kigoma. Unaweza ukajiuliza Kigoma kuna nini? Hili swali linatokana na kuwa licha ya Mkoa wa Kigoma kuwa na rasilimali na fursa nyingi za kiuchumi, umekuwa ukishika nafasi za mwisho katika ripoti mbalimbali za utafiti zinazotolewa Tanzania.
Mkoa huo ambao umepakana na nchi za Burundi na Mkoa wa Kagera upande wa Kaskazini, mikoa ya Geita na Tabora upande wa Mashariki na Mkoa wa Rukwa upande wa Kusini katika ripoti ya hali ya malaria iliyotolewa Oktoba, umeonyesha ulivyo katika hali mbaya kwa watoto wa chini ya miaka mitano.
Katika ripoti hiyo ya Matokeo ya Utafiti wa Viashiria vya Malaria Tanzania 2017 uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na kuzinduliwa mwezi huo, Kigoma inaongoza kwa maambukizi ya ugonjwa huo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kwa asilimia 24.4.
Kinachoshangaza ni kuwa Kigoma ndiyo mkoa unaoongoza kwa watoto wanaolala kwenye neti zilizowekewa dawa kwa asilimia 61.1 kwa mujibu wa Ripoti ya Hali ya Malaria 2017 iliyotolewa na NBS, mwaka huu.
Hata hivyo, matokeo hayo yanaonyesha kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo kitaifa yamepungua kutoka asilimia 14.4 mwaka 2015 mpaka asilimia 7.3 mwaka 2017, huku Wilaya ya Kakonko iliyopo mkoani humo ikiongoza kwa maambukizi kwa asilimia 30.8.
Matokeo hayo hayana tofauti sana na matokeo mengine yaliyotangazwa Aprili 25 mjini Kasulu, Kigoma na NBS yakionyesha mikoa 10 kati ya 26 ya Tanzania Bara ina viwango vikubwa vya maambukizi ya malaria. Katika mikoa hiyo, Kigoma imeongoza kwa asilimia 24.4 ikifuatiwa na Geita 17.3, Kagera asilimia 15.4, Mtwara asilimia 14.8 na Ruvuma asilimia 11.8.
Pia, Kigoma ndiyo mkoa unaongoza kwa umaskini nchini.
Ukiacha kuongoza kwa maambukizi ya malaria mkoa huo pia unaongoza kwa umaskini.
Taarifa ya Hali ya Uchumi ya 2015 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2016/17 iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ilionyesha kuwa mkoa huo unaongoza kwa umaskini kwa asilimia 48.9 kutokana na Sensa ya Watu na Makazi ya 2012.
Mikoa mingine yenye umaskini wa kipato na kiwango chake katika mabano ni Geita (asilimia 43), Kagera (asilimia 39), Singida (asilimia 38.2) na Mwanza (asilimia 35.3).
Mbali na umaskini wa kimkoa, Wilaya ya Kakonko iliyomo mkoani humo ndiyo inaongoza kwa umaskini nchini ikifuatiwa na ya Biharamulo mkoani Kagera, ambapo Dk Mpango alisema katika wilaya hizo takriban asilimia 60 ya watu wake wako chini ya mstari wa umaskini wa mahitaji ya msingi.
Tathmini ya hali ya umaskini kimaendeleo iliyoainisha umaskini huo, imetumia takwimu za Sensa ya Watu ya mwaka 2012 na Utafiti wa Hali ya Kipato na Matumizi katika Kaya wa 2012, ulionyesha pia ahueni ya umaskini katika mikoa mitano.
Pamoja na umaskini wa kipato, mkoa huo haujabaki salama kwenye ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali(CAG), kwani umeonekana ukipata hati zisizoridhisha kwa miaka minne mfululizo kutoka 2014/15 hadi 2017/18.
Ripoti ya CAG ya 2016/17 iliitaja Hamashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji ambayo inapata hati chafu kwa mwaka wa tatu mfululizo ikitumia zaidi ya Sh22 bilioni alizohoji matumizi yake pamoja na kushindwa kurekebisha makosa ya miaka iliyopita.
Ripoti hiyo pia imezitaja pia halmashauri za wilaya za Kigoma na Pangani, hatua iliyomfanya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo kuwasimamisha kazi wakurugenzi wawili kati ya watatu wa halmashauri za Pangani na Kigoma.
Baadhi ya wadau wamejadili suala la umaskini wa mkoa huo wakitaja sababu na kutoa suluhisho walipokuwa wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe anasema umaskini wa mkoa huo ni wa kutengeneza, lakini kwa uhalisia hakuna umaskini.
“Kigoma inaonekana kwenye takwimu kwamba watu wake wana kipato kidogo, lakini kwenye uhalisia ni mkoa ambao haujawahi kulia njaa. Kwa maana shughuli za uchumi hazirekodiwi kwenye takwimu, wanaita off market,” alisema Zitto.
“Tuna lishe ya kutosha kutoka kwenye samaki, tuna chakula cha kutosha kwa sababu ya hali ya hewa. Kwa hali halisi sisi siyo maskini kwa sababu tunaweza kujilisha, lakini kwa takwimu za Serikali sisi ni maskini kwa sababu shughuli zetu za uchumi siyo rasmi, hazirekodiwi.”
Mbali na kuamini hivyo, Zitto anauona mkoa huo umetengwa kwa kutounganishwa na barabara za lami. “Wilaya inayozalisha chakula kwa wingi ni Kasulu, lakini barabara inayotoka huko kuja Kigoma, bado haijakamilika miaka sita sasa. Wilaya za Kakonko na Kibondo kufika ni shida,” alisema mbunge huyo.
“Kwa mara ya kwanza tumeona daraja la Malagarasi, lakini bado kuna kilometa zaidi ya 100 ni vumbi. Kwa hiyo tumekuwa kama kisiwa, hakuna shughuli za kutosha za uchumi.”
Pia, alitaja kudorora kwa usafiri wa reli na hatimaye bandari kufa kwa kukosa mizigo kuwa sababu mojawapo ya kuongezeka kwa umasikini.
“Hatuna viwanda kwa sababu hatuna umeme wa gridi ya Taifa, tunatumia umeme wa mafuta. Tuna ziwa lakini hatuna viwanda vya samaki kama Mwanza na Mara. Kihistoria kulikuwa na sera ziliitenga Kigoma na kuwa pembezoni.”
Zitto anashauri kuongezwa kwa kuongeza shughuli za kiuchumi ikiwamo kuboresha bandari ya Kigoma. “Sisi tuna mradi unaitwa Ujiji City ambao unalenga kuwawezesha wafanyabiashara wa Congo na Burundi wanaokwenda kuchukua mzigo China ule mzigo upitie hapa, bandari waulete bandari kavu ili shughuli ziongezeke. Tayari tenda imeshatangazwa,” alisema.
“Mbali na Lubumbashi, kuna miji ya Kalemie, Moba, Baraka, Bukavu na Uvira ya Congo kote kuna watu 25 milioni wanaotegemea Kigoma.”
Kuhusu uvuvi, Zitto alisema asilimia 30 ya wakazi Kigoma wanaitegemea sekta hiyo, hivyo wameanza kuboresha maeneo ya wavuvi. “Tumepata msaada wa Denmark pale Kibirizi kuna eneo la kuboresha uvuvi na eneo jingine ni Buhigwe japo lenyewe hatujapata mfadhili,” alisema mbunge huyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mwaliwa Pangani anasema mkoa unaendelea kuwa maskini kwa sababu wananchi hawatumii fursa zilizopo ipasavyo.
Anatoa mfano wa fedha za mikopo zilizopo ofisini kwake akisema vijana na wanawake hawazichangamkii licha ya kuhamasishwa.
“Mimi mwenyewe nimetangaza kuwa nina fedha za kutoa mikopo, lakini kati ya viku 32 vilivyoomba mikopo, ni vikundi viwili tu vya vijana ndiyo vimeomba. Hawajitokezi kutumia fursa hizo,” alisema Pangani.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali mstaafu Emmanuel Maganga anasema hali ya usalama kwa mkoa huo iko vizuri akiwataka wawekezaji kutohofia kwenda kuwekeza.
“Tangu mwaka 2014 tumeimarisha usalama, tumeongeza kambi za jeshi mipakani na tunafanya operesheni. Yale mambo ya utekaji mabasi hayapo tena,” alisema Brigedia Jenerali mstaafu Maganga.
Alisema uhalifu uliopo kwa sasa ni mdogo unaoshughulikiwa na vyombo vyabulinzi na usalama.