Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kigoma kuwa kitovu cha biashara

Fri, 10 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kigoma. Mkoa wa Kigoma unaweza kutumika kama kituo kikuu cha biashara katika ukanda wa nchi zinazozunguka ziwa Tanganyika na watu kutoka nchi jirani kununua bidhaa mkoani humo.

 

Kauli hiyo imetolewa na mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geofrey Mwambe leo Alhamisi Mei 9, 2019 wakati akizungumza katika kongamano la biashara linalofanyika mkoani humo.

 

Kongamano hilo linahusisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Tanzania, Zambia, DRC, Burundi na Rwanda ambako wanajadili njia bora ya kuboresha biashara na kukuza uchumi.

 

"Kigoma inaweza kutumika kama kitovu cha biashara kwenye nchi za maziwa makuu hususani kwenye maeneo ya uwekezaji mkubwa na mdogo, utalii na biashara.”

 

“Unaweza kutumika kama soko kubwa na wafanyabiashara kutoka nje na watu wakaja kununua bidhaa hapa badala ya kwenda Dubai au China, na hilo linawezekana endapo tutaamua kufanya hivyo," amesema Mwambe.

 

Mwambe ametoa wito kwa wawekezaji kwenda Kigoma kutokana na kuwa na fursa nyingi za uwekezaji hususani kwenye kilimo, utalii, ujenzi wa viwanda na biashara.

 

Mkuu wa mkoa Kigoma, Emanuel Maganga amesema Mkoa huo umejipanga kuhakikisha fursa za uwekezaji na biashara zinatumika ipasavyo na uchumi unakuwa kwa kasi.

 

"Wawekezaji njooni Kigoma kuna fursa nyingi na nzuri kwani ardhi ipo ya kutosha na yenye rutuba, miundombinu ya usafiri na usafirishaji ipo vizuri na barabara nyingi sasa zinajengwa kwa kiwango cha lami, kiwanja cha ndege kipo," amesema Maganga.

 

Naibu waziri wa Tamisemi,  Josephart Kandege amesema kauli mbiu ya "mipaka yetu na maendeleo" ikitumika vizuri itasaidia kuinua uchumi katika nchi za maziwa makuu.

 

Amesema uchumi imara utakuwa kichocheo cha kuanzisha viwanda vikubwa na hivyo fursa za kiuchumi kuongezeka kwa watu wa ukanda wa maziwa makuu.

 

"Hii mipaka tuliwekewa na wakoloni lakini isiwe kikwazo kwa wananchi kushirikiana na wenzao katika nchi jirani kufanya biashara, muhimu tu ni kufuata utaratibu uliowekwa kisheria," amesema Kandege.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz