Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kigoma: Maaskofu wakemea utoaji uchawi majumbani

Uganga Uchawiii Kigoma: Maaskofu wakemea utoaji uchawi majumbani

Tue, 6 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MAASKOFU na wachungaji mkoani Kigoma wameungana kupaza sauti zao kupinga vitendo vya utoaji uchawi kwenye nyumba za wananchi unaoendelea mkoani humo maarufu kama Lambalamba au kamchape.

Mwenyekiti wa Jumuia ya Kikristo (CCT) Mkoa wa Kigoma kutoka kanisa Anglikana jimbo la Magharibi, Sospeter Ntemelwa Ndenza amesema hayo akizungumza kwa niaba ya maaskofu na wachungaji wa makanisa ya Mkoa Kigoma ambao wamelaani jambo hilo.

Maaskofu na wachungaji hao wametangaza azimio la pamoja kupita kwenye makanisa yote kutoa elimu kwa waumini wao kuhusu madhara ya vitendo hivyo na namna vinavyoleta athari kwa jamii.

Askofu Ndenza alisema kuwa viongozi hao wa dini hawaigopi uchawi na hawauamini na kwamba watatumia nafasi yao kueleza jambo hilo kwa waumini hasa suala la sheria za nchi lakini pia masuala hayo ya uchawi yanavyopingana na imani na vitabu vya dini.

Akizungumza baada ya tamko hilo la maaskofu Mkuu wa mkoa Kigoma, Thobias Andengenye ameshukuru maaskofu hao kwa azimio lao la kuunga mkono vitendo vya kupinga kutoa uchawi kwenye nyumba za watu (Kamchape) kwani vimeleta madhara makubwa kwa jamii.

Andengenye alisema kuwa serikali imekuwa ikileta fedha nyingi kwa ajiili ya utekelezaji wa miradi lakini mambo hayo hayataweza kufanyika vizuri kama hakutakuwa na amani hivyo serikali inasimamia kwa karibu kulipiga marufuku na kulidhibiti suala hilo la kamchape.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa madhara yameshatokea kwa sababu ya vitendo hivyo ikiwemo vifo,kuchomwa kwa mali za watu, mali za serikali na kwa sasa zaidi ya watu 200 wamekamatwa na kufikisha mahakamani kwa ajiili ya hatua za kisheria.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live