Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kujengwa kwa kiwango cha lami kwa barabara zenye urefu wa kilomita 41 wilayani ya Kigamboni.
Akitoa salamu za Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha kuunganisha malori na matipa cha Saturn kilichopo Kigamboni mkoani Dar es Salaam, Chalamila amesema kilio cha muda mrefu cha ubovu wa barabara katika wilaya hiyo kimepatiwa ufumbuzi.
Chalamila amezitaja barabara zitakazojengwa ni pamoja na barabara ya Kibada -Mwasonga yenye urefu wa kilomita 15.6, Mwasonga - Kimbiji Songani kilomita 10, Kimbiji Songani - Kijaka kilomita 8.5, Kimbiji - Cheka kilomita 7 na Kijaka - Kimbiji kilomita 5.
Ameongeza kuwa katika mradi wa uendelezaji miundombinu ya wa Mkoa wa Dar es Salaam (DMDP) Serikali imetenga shilingi Bilioni 88 kujenga barabara zenye urefu wa kilomita 42 kwenye wilaya ya Kigamboni pekee.