Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kifahamu Kijiji cha Lupaso na asili ya ukoo wa Wakapa

4f02347365fe1937a2d8bdd8db1c5743 Kifahamu Kijiji cha Lupaso na asili ya ukoo wa Wakapa

Fri, 14 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

LUPASO ni kijiji cha asili chenye mchanganyiko wa watu wa ukoo wa Wamwale (Wayao) waliotokea nchini Malawi na ukoo wa Wakapa waliotokea nchini Msumbiji wakiongozwa na Chifu Mkonona wa Kwanza.

Asili ya jina Wakapa (Mkapa) ni neno la Kimakua lenye maana ya mnyama kobe na kwa Kimakua maana yake ni Kapa. Wamakua (Wayao) hugawanyika kwa koo hivyo ukoo wa Wakapa unaongozwa na Chifu Mkonona kati ya machifu wengi wa kabila hilo kwa kila ukoo.

Tangu kuwe na Chifu Mkonona wa kwanza mpaka sasa, kumeshakuwa na machifu hao watano. Chifu Mkonona wa Tano ndiye aliyelieleza gazeti hili, historia ya kuanza kwa kijiji hicho chenye wakazi takribani 2,000.

"Mababu zetu walichagua Lupaso kuwa makao yao ya kudumu. Chifu Mkonona wa kwanza alipowafikisha hapa, yeye alirudi Msumbiji. Chifu Mkonona wa pili tulimzika hapa hapa kijijini," anasema Chifu Mkonona akieleza historia hiyo ni ya kabla ya mwaka 1920.

Anasema baadaye, koo nyingine ikiwemo yenye machifu waitwao Mripa, Wamwale na Mkonona, walizunguka katika maeneo kutafuta hifadhi za kutosha kwa watu wao, wengine walichagua milimani na wengine chini ya milima, ndipo Mkonona alipochagua eneo hilo.

"Historia zinaeleza kuwa nyakati zile hakukuwa na fedha taslimu katika kununua au kuuza vitu, watu walikuwa wakifanya biashara kwa mtindo wa kubadilishana vitu kwa vitu. Mazao hayakuwa pesa. Alipokuwa akiishi kiongozi kulikuwa na mlima kama kofia, watu wenye mazao walipenda kupumzika hapo, palikuwa mahali pa kukutania kwa biashara.”

"Hapo ndipo lilipoanzia jina Lupaso kwani Wazungu walipofika hapo, waliwasikia wenyeji wakisema kwa kilugha 'Ulika rupa sho' wakimaanisha mahali hapo ukijaribu kulala unakosa usingizi kwa kuwa unawaza mlima huo utakuangukia, wakashindwa kutamka kama walivyotamka wenyeji ndio wakaishia kusema Lupaso," anaeleza Chifu Mkonona.

Anasema wakazi wa kijiji hicho ni cha wakulima zaidi ingawa wapo wanaofuga kidogo mbuzi, ng'ombe na nguruwe wachache.

Wengi wa wakazi wa hapo wanalima mahindi, mihogo kama mazao ya chakula, ufuta, korosho, mbaazi, kunde na njugu kama mazao ya biashara.

Mama mdogo wa Mkapa, Rose Magnus Mkapa (94), anathibitisha kauli ya Chifu Mkonona kuwa kijiji hicho chenye umbali wa zaidi ya kilometa 30 kutokea Masasi mjini, ni cha asili na wenyeji wa mwanzoni kabisa ni ukoo wa Mkapa.

"Kijiji cha Lupaso kilianzishwa na ukoo wa Mkapa pekee wakiishi ndugu wa familia moja kwa malezi lakini baada ya uhamisho wa vijiji vya ujamaa, walihamia watu kutoka maeneo mengine na kutengeneza jamaa moja tulio nayo mpaka leo," anasema mama mdogo Rose aliyezaliwa mwaka 1926.

Mtendaji wa Kijiji cha Lupaso, Raphael Mlaponi, anasema kuwa, kijiji hicho kina watu 2,755, watu wazima (wenye uwezo wa kufanya kazi) wakiwa 1,897 na waliobaki ni watoto.

Kiuchumi, hali ya uchumi si nzuri kutokana na upungufu wa maji unaosababisha ukame. Kijiji hicho kipo katika mwinuko na wenyeji wanasema mvua ikinyesha maji yote hutiririka katika Mto Ruvuma na ardhi yao hukauka mapema.

Mlaponi anasema wananchi wa Lupaso wengi wakiwa ni wa kabila la Wayao na Wamakua wachache, wanategemea mazao ya korosho na mbaazi kwa biashara na mahindi na mtama kwa chakula.

Kwa mujibu wa Mlaponi, ukubwa wa kijiji hicho kwa upande wa Kaskazini ni kilometa 52 hadi kijiji kingine, Mashariki ni kilometa 68, Kusini zipo kilometa 42.

Ukitoka Lupaso hadi kufika nchi jirani ya Msumbiji, utapaswa kuvivuka vijiji vinne na cha Lupaso cha tano. Vijiji hivyo kuanzia cha kwanza baada ya Lupaso hadi cha mpakani ni Mtojo, Utinde, Myesi na Mbangara ambacho ndicho kijiji cha mpakani kabisa mwa Tanzania na Msumbiji kinachotenganishwa na Mto Ruvuma.

"Hapa kijijini tuna ushirikiano mkubwa, tunaishi kama jamaa moja. Wapo watu wa imani tofauti na kila mtu anaabudu kwa uhuru na haki. Lakini pia, usalama ni mkubwa na mzuri sana, tuna kikundi cha sungusungu katika kila kitongoji watu watatu watatu," anaeleza Mlaponi.

Lupaso ina shule moja ya msingi ambayo ndiyo alikosoma Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin Mkapa.

Ina shule moja pia ya sekondari, hii hakusoma kwa kuwa baada ya kumaliza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Lupaso, alichaguliwa kwenda kusoma Shule ya Sekondari ya misheni (ya Kanisa Katoliki) ya Ndanda.

Mtendaji wa Kijiji anasema wapo katika mchakato wa kukusanya michango ili waanze ujenzi wa zahanati ya Kijiji. Anasema kwa sasa wanapata huduma za afya katika Zahanati ya Kanisa Katoliki iliyopo kijijini hapo na wanaishukuru kwa huduma nzuri.

Usafiri wa umma kutoka mjini Masasi hadi Lupaso upo. Wananchi na wageni hupata usafiri wa mabasi mawili. Moja huanza safari zake saa 1:30 asubuhi na lingine saa mbili asubuhi kwenda Masasi.

Mabasi haya kufanya safari mara mbili kwa siku kutokana na idadi kidogo ya wasafiri inayowalazimu kusubiri muda mrefu na kupunguza idadi ya safari.

Masasi ni mji wa kibiashara, umechangamka mchana kwa usiku. Wakati wa msiba wa Mkapa, nyumba za kulala wageni na hoteli zote za Masasi zilijaa wageni na kusababisha uongozi wa mkoa kupitia Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa, kutangaza maeneo mengine watakakofikia wageni.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, pamoja na kwamba kijiji cha Lupaso kina makazi bora, lakini hakina nyumba ya kulala wageni na ingawa baadhi ya nyumba za familia ya Mkapa ikiwamo alikozaliwa na kukulia Mkapa, wageni walifikia humo.

Wageni wengine walishukia Mtwara mjini umbali wa kilometa 225 mpaka kijijini Lupaso na wengine walilala Newala ambako ni umbali wa kilometa 51 hadi kijijini huku wageni wengine wakishukia Nachingwea ambako ni kilometa 83 mpaka kijijini Lupaso.

Barabara aliyozawadiwa Mkapa wakati akiwa hai na Rais Magufuli ya kilometa 11 ni alama ya upendo kwa wanakijiji wa Lupaso kwa Serikali yao, ingawa kilio chao kikubwa hivi sasa wanachoomba serikali iwasaidie ni maji ya uhakika na kuboresha mawasiliano ili kuchochea maendeleo yao.

Dk Joseph Mkapa anayemuita Benjamin Mkapa mjomba, alisema wakati mwingine mjomba wake huyo alishindwa kukaa Lupaso kutokana na tatizo la mawasiliano na kuishi muda mwingi Masasi mjini ambako pia amejenga makazi yake tangu mwaka 1986.

"Kipindi cha zamani hapa walifunga mnara wa Airtel, lakini bado mawasiliano yamekuwa shida sana. Katika kipindi hiki cha ulimwengu wa mtandao, tunaiomba Serikali iliangalie hili kwa kuwezesha minara ifungwe hapa ikiwa pia ni sehemu ya kumuenzi Mzee," alieleza Dk Mkapa alipozungumza na gazeti hili kijijini hapo.

Wakazi wa Lupaso ni wakarimu, wanyenyekevu, waliojaa upendo kwa wageni na kati yao, wanaishi kama ndugu na wamedhamiria kumuenzi Mkapa kwa vitendo kwa kufanya kazi kwa bidii zaidi ya awali kama kaulimbiu aliyopenda kuwaeleza Mkapa alipokuwa hai hapa duniani.

Chanzo: habarileo.co.tz