Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiboko auawa Moro, wananchi wapewa kitoweo

9546 Kiboko+pic TZWeb

Wed, 20 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Kiboko aliyeonekana karibu na makazi ya watu, eneo la Kihonda, Morogoro, ameuawa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama pori (Tawa) na wananchi wakagawiwa kitoweo.

Kiboko huyo mwenye uzito wa kilo 2,300, alionekana katika eneo hilo jana alfajiri na kuzua taharuki miongoni mwa wananchi wa eneo hilo.

Hata hivyo, Ofisa Mwandamizi wa Tawa, Privatus Kasisi alisema walilazimika kumuua kwa kuwa alionekana kuwa na hasira baada ya wananchi kumsumbua na kumpigia kelele.

Alisema baada ya kumuua walilazimika kumkata kichwa halafu kiwiliwili chake tulikipeleka ofisi ya Kata ya Kihonda na kukikabidhi kwa uongozi kwa ajili ya kuwapa wananchi kitoweo.

“Sisi kazi yetu tulishamaliza ya kuhakikisha wananchi hawapati madhara yoyote wala kujeruhiwa na sasa tumeukabidhi uongozi wa kata wao watajua wamfanye nini, sisi tuliondoka na kichwa tu kwa ajili ya uchunguzi wetu,” alisema Kasisi.

Alifafanua kuwa kiboko huyo alipotea miaka 20 iliyopita akitokea Mto Wami.

Mkazi wa Kata ya Kihonda, Michael Waitara alisema kuonekana kwa wanyama kama hao kwenye maeneo ya makazi ya watu kunazua hofu.

“Huyu mnyama alitaka kusababisha maafa kwa watoto wawili wanafunzi waliokuwa wakienda shule kwani walidhani ni ng’ombe na walikuwa wakimshanga na yeye akawa anawafuata, ndipo nilipowaeleza waondoke kwa sababu huyo ni mnyama hatari,” alisema Waitara.

Mkazi mwingine wa Kihonda, Bahati Mangeli aliiomba mamlaka ya wanyama pori kuwa na utaratibu wa kuzipitia njia za wanyama mara kwa mara ili kudhibiti uingiaji wa wanyama hao kwenye makazi ya watu.

Chanzo: mwananchi.co.tz