Kesi ya Jinai Na 08 ya Mwaka 2023 iliyokuwa inamkabili Askari wa Jeshi la Polisi H.4178 Abati Benedectio wa Kituo cha Polisi Bariadi Mkoani Simiyu kutuhumiwa kumpiga hadi kumjeruhi vibaya mtoto wake mwenye umri wa miaka 7 (jina linahifadhiwa) imerejeshwa tena.
Askari hiyo Februari 17, 2023 alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Bariadi, kujibu tuhuma zilizokuwa zinamkabili, ambapo baadaye ilifutwa Mei 22, 2023 kwa madai mashahidi upande wa Jamhuri kushindwa kufika Mahakamani mara tatu mfululizo.
Kabla ya kufutwa, Askari huyo alisomewa Mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Mariamu Nyangusi na mwendesha Mashitaka wa Serikali kwa wakati huo, Daniel Masambu.
Masambu alieleza kuwa mtuhumiwa alimchapa mtoto wake kwa fimbo na kumjeruhi maeneo mbalimbali ya mwili wake kinyume na Kifungu cha 169 A Kifungu Kidogo cha 1 na cha 2 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura 16 marejeo ya Mwaka 2022.
Kesi hiyo ilifutwa kwa kile kilichoelezwa kuwa mashahidi kushindwa kufika Mahakamani mara tatu mfululizo kutoa ushahidi.
Majibu ya kuwa mashahidi hao hawapo yalitolewa na Jeshi la Polisi upande wa upelelezi katika Ofisi ya Mashitaka Mkoa baada ya kupelekewa hati tatu za kuitwa shaulini (Samas) mashahidi watatu ambao walikuwa ni Mtoto mwenyewe, Mama mzazi wa mtoto pamoja na mama Mlezi wa mtoto.
Ofisi ya Mashitaka ilieleza kuwa Hati zote 3 zilijibiwa na Jeshi la Polisi, kuwa mashahidi wanaohitajika hawapo Bariadi na hawajulikani walipo, ndipo kesi ikafutwa.
Hata hivyo sababu hizo zilionekana kuwa hazina ukweli, kwani mashahidi wote waliokuwa wanahitajika walikuwa wanapatikana na wanaishi Mjini Bariadi ambapo baadhi ya mashahidi hao walisema hawajawahi kupata barua ya wito kuwa wanahitajika Mahakamani.
KESI YAREJESHWA TENA Kesi hiyo imerudishwa tena Septemba 22, 2023, ikiwa imepita miezi mitatu tangu kufutwa ambapo imekuja kama kesi mpya Jinai Namba 59, 2023 na wameanza kusikilizwa mashahidi wa upande wa Jamhuri.
Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Caroline Kiliwa wamesikilizwa mashahidi wawili kati ya tisa watakaotoa ushahidi, ambapo waliotoa ushahidi ni mtoto mwenyewe pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Bariadi wakati huo, SSP Piter Ntinginya.
Baada ya kusikilizwa kwa Mashahidi hao, Hakimu ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 12, 2023 kesi ikapoendelea kusikilizwa tena.