Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya aliyehukumiwa kunyongwa, kusikilizwe tena kisa Lugha

MAHAKA HI 1 Law Kesi ya aliyehukumiwa kunyongwa, kusikilizwe tena kisa Lugha

Fri, 21 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Rufani Kanda ya Shinyanga, imeamuru kesi ya mauaji inayomkabili, Juma Ndodi, aliyehukumiwa kunyongwa, ianze kusikilizwa upya kwa sababu hoja za awali na maelezo ya mashahidi yalisomwa kwa Lugha ya Kiswahili wakati yeye anaelewa Kisukuma.

Uamuzi huo ulitolewa mbele ya jopo la majaji watatu, Jaji Augustine Mwarija, Ignas Kitusi na Agnes Mgeyekwa waliosikiliza rufani iliyowasilishwa na Ndodi akipinga hatia na adhabu ya kunyongwa hadi kufa aliyopewa na Mahakama Kuu.

Jopo hilo katika uamuzi wao, walikubaliana na hoja za mawakili wa pande zote mbili kuwa mrufani alikuwa na haki kuelewa shtaka na aina ya ushahidi atakaokutana nao wakati wa usikilizwaji kesi.

“Mrufani hakuwa anaelewa lugha iliyotumiwa na mahakama, hakuna ubishi kwamba alinyimwa haki yake na hivyo hawawezi kusema kuwa mlolongo wa usomwaji wa maelezo ya mashahidi ulifanyika kwa usahihi,” lilisema jopo.

Mahakama ilibainisha kwamba, mahakama ya chini haikutoa mkalimani kwa mrufani hali ambayo imemnyima haki ya kujua aina ya shtaka linalomkabili na ushahidi ambao upande wa mashtaka unatarajia kuutumia kwa maana hiyo mlolongo huo ulikuwa na dosari. “Kwa dosari zilizojitokeza tunabatilisha mlolongo wa usomwaji wa maelezo ya mashahidi wa mahakama ya chini na Mahakama Kuu, tunafuta hatia na hukumu ya Mahakama Kuu.

“Kwa minajili ya maslahi ya haki, Mahakama inaamuru kesi hiyo isikilizwe upya kuanzia hatua ya kusomwa maelezo ya mashahidi na awepo mkalimani, mrufani abaki mahabusu,” lilisema jopo hilo.

Katika kesi hiyo, ilidaiwa Februari 27, 2015, Kijiji cha Buyange Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga alimuua Modester Kilijiwa.

Alisomewa shtaka lake katika Mahakama ya Wilaya ya Kahama Machi 12, 2015, bila kuwapo mkalimani na Februari 3, 2016 kesi hiyo ilianza kusikilizwa Mahakama Kuu Shinyanga bila mkalimani huku yeye akiwa anaelewa lugha ya Kisukuma pekee.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live