Mahakama Kuu, kanda ya Dar es Salaam, imepanga kusikiliza shauri la jinai, lililofunguliwa na mwanahabari mahiri nchini, Saed Kubenea, dhidi ya Paul Makonda, aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam.
Katika kesi hiyo, namba 151 ya mwaka 2022, Kubenea anaiomba Mahakama Kuu imruhusu kumfungulia shauri la jinai Makonda, kwa kile alichokiita, “kuisaidia serikali kutimiza wajibu wake.”
Anasema, Makonda ametenda makosa kadhaa wakati akiwa madarakani, lakini serikali kwa makusudi, imeamua kunyamazia matendo ya kiongozi huyo, kinyume na Katiba ya Jamhuri na sheria nyingine za nchi.
Kesi dhidi ya Makonda, imepangwa kusikilizwa tarehe 7 Machi mwaka huu, saa mbili asubuhi, mbele ya Jaji Salma Magimbi.
Miongoni mwa tuhuma anazodaiwa kuzitenda Makonda, ni matumizi mabaya ya madaraka, ikiwa kuvamia kituo cha televisheni cha Clouds, akiambatana na askari waliobeba bunduki.
Makosa mengine, ni ukiukwaji wa haki za binadamu, kujimilikisha kinyume cha sheria, mali mbalimbali yakiwamo mashamba na viwanja, kima vile kiwanja namba 60 kilichopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Mapema mwaka jana, Kubenea alifungua shauri la jinai kama Miscellaneous Criminal Application Na. 1 ya mwaka 2022 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, akitaka mahakama hiyo, kumruhusu kumshitaki mwanasiasa huyo.
Hata hivyo, mahakama ilitupia mbali maombi hayo kwa madai kuwa hati ya mashitaka inaonyesha makossa yaliyotendwa, mamlaka yake ni Mahakama Kuu.
Kubenea amepinga uamuzi huo, uliotolewa na Hakimu Mkazi, Aron Lyamuya, kwa maelezo kuwa alichokijadili Hakimu siyo kilichopo mahakamani.
Alisema, Hakimu Lyamuya amejadili hati ya mashitaka, wakati shauri lililopo mahakamani, lilikuwa kuomba ruhusa ya kufungua mashitaka.
Makonda anadaiwa kuwa siku ya tarehe 17 Machi 2017, akiwa na watu waliobeba silaha za moto, alivamia Clouds TV na kumuagiza mtangazaji wa kipindi cha Shilawadu, kurusha video inayomwonesha mwanamke aliyejulikana kwa jina la Grace Athuman.
Katika video hiyo, ambayo haijulikani nani ameiandaa, mwanamke huyo alidaiwa kuonekana akifanya tendo la ndoa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.
Kwa mujibu wa ushahidi wa video za CCTV, Makonda anaonekana kuvamia kituo cha Clouds saa nne usiku, akiwa anaendesha mwenyewe gari namba T553BFM.
Vilevile, Camera za CCTV pamoja na kitabu cha kumbukumbu za walinzi, vinamuonesha Makonda aliingia Clouds akiwa na askari wanne waliokuwa na sare tofauti za majeshi ya ulinzi na usalama, kati yao watatu wakiwa na silaha za moto.
Askari hao waliingia hadi chumba cha utangazaji, jambo ambalo ni kinyume na kanuni za utangazaji, huku Makonda akitumia vitisho dhidi ya wafanyakazi wa Clouds kwa kutumia silaha za moto.
Kwa mujibu wa hati ya kiapo ya Kubenea, kitendo cha Makonda cha kuvamia televisheni ya Clouds, tena akiwa ameongozana na askari waliobeba silaha za moto, ni kinyume cha sheria ya Kieletroniki na Posta ya mwaka 2010.
Wakili Hekima Mwasipu
Maombi ya kutaka kumshitaki Makonda yamewasilishwa mahakamani, chini ya kifungu cha 99 (1) cha Sheria ya mwenendo wa mashauri ya Jinai, Sura ya 20.
Kubenea ambaye amewahi kuwa mbunge wa Chadema katika jimbo la Ubungo, katika Bunge lililopita anasema, hatua ya Makonda kuvamia Clouds, ni matumizi mabaya ya madaraka, chini ya kifungu cha 96 ya Kanuni ya adhabu (Penal Code), Sura ya 20 na kuingilia moja kwa moja, mawasiliano ya Kieletroniki.
Mbali na Makonda, wengine walioshitakiwa ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Wawili hawa wanadaiwa wameshindwa kuchukua hatua za kumfungulia mashitaka ya jinai mtuhumiwa huyo.
Katika kujenga hoja yake mahakamani, wakili wa Kubenea ameambatanisha ripoti ya uchunguzi ya Kamati Maalum iliyoundwa na aliyekuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye.
Ripoti ya Nape iliyochunguza tukio la kuvamiwa Clouds, ilimtia hatiani Makonda na kupendekeza kwa mamlaka yake ya uteuzi, kumchukulia hatua za kinidhamu; Makonda mwenyewe kuwajibika binafsi na kuwaomba radhi Clouds na wananchi kwa ujumla.
Hata hivyo, mapendekezo yote ya Kamati ya Serikali hayakutekelezwa. Muda mfupi baada ya Nape kumaliza kusoma ripoti yake kwa waandishi wa habari, Rais John Magufuli alitangaza kumfuta kazi.
Nape amerejea kwenye baraza la mawaziri, baada ya Magufuli kufariki na Rais Samia Suluhu Hassan, kuchukua madaraka.
Kamati ya Nape ilithibitisha kuwa Makonda alivamia kituo hicho cha televisheni akiwa anaendesha mwenyewe gari lenye namba T553 BFM na kuingia hadi chumba cha utangaji, jambo ambalo ni kinyume na kanuni za utangazaji.
“Lengo siyo kushinda tu. Kesi hii, inalenga kuzionyesha mamlaka za kuendesha mashitaka ya Jinai (DPP), kwamba kuna mtuhumiwa mmoja anastahili kuburuzwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili. Lakini hawajaweza kufanya hivyo na kunyamaza kwao, ni kuvunja Ibara ya 59 (B) Ibara ndogo ya (4) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano,” ameeleza Kubenea.
Alisema, “hata mataifa makubwa kama Marekani, yamewahi kumuwekea vikwazo vya kwenda nchini humo Makonda na familia yake, kutokana na tuhuma za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
“Pamoja na Marekani kuwa taifa mshirika na Tanzania kwenye mambo kadhaa kihistoria, pamoja na uwezo wa Marekani kuweza kutambua mambo mbalimbali yanayotokea duniani, lakini serikali imeshindwa kufanyia kazi taarifa ya Marekani kuhusiana na matendo ya Makonda.”
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, 31 Januari 2020, ilieleza kuwa serikali ya nchi hiyo, imempiga marufuku Makonda na mke wake, Mary Massenge, kufuatia tuhuma za ukandamizaji wa haki za wananchi; kunyima watu haki ya kuishi, haki ya uhuru wa kujiamulia mambo na usalama wa watu.
“Wizara ina taarifa za uhakika kuwa Makonda amehusika katika uvunjifu huo wa haki kupitia nafasi yake kama Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Katika nafasi yake hiyo, pia amelaumiwa kwa kukandamiza upinzani wa kisiasa, kukandamiza haki ya kujieleza, na kushambulia makundi yasiyo na sauti,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Michael Pompeo alitumia mtandao wake wa Twitter kutangaza marufuku hiyo.
Alisema, “…leo tumetangaza kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Christian Makonda, hataruhusiwa kuingia Marekani, kutokana na kushiriki kwake katika ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.”
Katika kesi hiyo, Kubenea anawakilishwa mahakamani na Hekima Mwasipu.