Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi waliopotea, kuuawa yaanza, DPP aweka pingamizi

Kesi Ya Dpp Dci Kesi waliopotea, kuuawa yaanza, DPP aweka pingamizi

Wed, 8 Feb 2023 Chanzo: Mwananchi

Shauri la watu waliokumbwa na madhila ya kupotea, kushambuliwa na kuuawa lililofunguliwa na mwanahabari, Luqman Maloto dhidi ya Serikali limeanza kupamba moto mahakamani baada ya kuanza kutajwa na kupangiwa tarehe ya usikilizwaji wa hoja za pingamizi la Serikali.

Maloto ambaye pia ni mwanaharakati wa haki za binadamu, amefungua shauri la maombi ya jinai Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam dhidi Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkurugenzi wa Mashataka (DPP).

Amechukua hatua hiyo kutokana na idara yenye dhamana ya upelelezi kushindwa kutoa taarifa za upelelezi wa matukio hayo yaliyowakumba baadhi ya watu wakiwemo wanahabari, wanasiasa na wasanii, kwa muda mrefu.

Shauri hilo linalosikilizwa na Jaji John Nkwabi limetajwa leo Jumatano, Februari 8, 2023 kwa mara kwanza ikiwa ni hatua ya awali ya kuelekea usikilizwaji wa hatima waathirika wa matukio hayo.

Hata hivyo, wakati shauri hilo likitajwa, mjibu maombi wa kwanza, DCI hakuwepo mahakamani wala mwakilishi au wakili wake, huku akionekana kutengwa mbali na uwakilishi wa mawakili wa Serikali.

Tofauti na ilivyo kawaida kesi inayoihusisha taasisi, idara, mamlaka au chombo chochote cha Serikali huwa kinawakilishwa na mawakili wa Serikali, lakini leo kwa mjibu maombi huyo wa kwanza ambaye ni mkuu wa idara ya Serikali ndani ya Jeshi la Polisi ilikuwa tofauti.

Mawakili wa Serikali waliofika mahakamani, Mutalemwa Kishenyi na Mwanaamina Kombakono wamejitambulisha kuwa wanamwakilisha mjibu maombi wa kwanza pekee, DPP na kumuacha DCI bila uwakilishi wowote.

Wakili wa mwombaji, Hekima Mwasipu ameieleza mahakama kuwa shauri hilo lilikuwa limepangwa leo kwa ajili ya kutajwa kwa mara ya kwanza na kwamba mjibu maombi wa kwanza alipelekewa wito wa mahhakama na afisa wa Mahakama.

Mwasipu amesema kuwa hata hivyo afisa huyo wa mahakama hakuwepo mahakamani kutoka uthibitishso huo ana akaomba mahakama ielekeze mjibu maombi huyo wa kwanza apelekewe tena wito wa kufika mahakamani.

Wakili Kishenyi ameieleza mahakama mjibu maombi wa kwanza (DPP) ameleta pingamizi la awali na kwamba wako tayari kwa usikilizwaji wa hoja hizo za pingamizi hilo huku akisema kuwa kutokuwepo kwa mjibu maombi wa kwanza hakuathiri chochote.

Hata hivyo wakili Mwasipu amepinga hoja hiyo akidai shauri hilo lilikuwa limepangwa kutajwa kwa mara ya kwanza na kwamba wajibu maombi hawajawasilisha majibu yao ya maandishi na kwamba hata hilo pingamizi walikuwa hawajapewa kama utaratibu wa kikanuni ulivyo.

Pia, amedai mjibu maombi wa kwanza hakuwepo (DCI) mahakamani na kwamba naye ana haki ya kusikilizwa, hivyo akaomba mahakama ielekeze mjibu maombi wa kwanza awapatie pingamizi hilo.

Ameiomba mahakama itoe hati ya wito kwa mjibu wa kwanza na mahakama ipange tarehe nyingine ya usiikilizwaji wa pingamizi hilo la awali.

Jaji Nkwabi amekubaliana na hoja za wakili Mwasipu na akaamuru DPP ampatie mwombaji pingamizi hilo, na wito utolewe kwa DCI kufika mahakamani na akapanga kusikiliza pingamizi hilo la awali la DPP Februari 22, mwaka huu.

Katika shauri hilo namba 5 la mwaka 2023, Maloto pamoja na mambo mengine anaiomba mahakama hiyo itamke kuwa DCI anawajibika kwa maisha ya watu aliowataja ambao wamo waliopotea, wlioshambuliwa na kuteswa na waliouawa, kwa kuwa wajibu wake ni kulinda maisha ya Watanzania.

Maloto amewataja waathirika hao ni pamoja mwandishi wa habari Azory Gwanda na wanasiasa Ben Saanane, Simon Kanguye, Daniel John, Tundu Lissu, Mdude Mpaluka Nyagali maarufu kama Mdude, Leopord Lwajabe, Akwilina Akwilini, Ibrahim Mshana maarufu kama Roma Mkatoliki na Allan Kiluvya.

Pia anaiomba mahakama hiyo itamke kuwa DCI ameshindwa ama kwa kutokuwa na uwezo au kwa maksudi kufanya upelelezi kuhusu madhila yaliyowakuta watu hao kutokana na kushindwa kutoa taarifa kwa uma na kwa familia za waathirika hao kuhusu madhila yaliyowapata.

Hivyo anaiomba pia mahakama hiyo itamke kuwa kwamba kuchelewa au kushindwa kukamilishwa kwa upelelezi dhidi yao hakuongozwi na kanuni yoyote, na itoe amri dhidi ya DCI kuwasilisha mahakamani hapo taarifa yenye maelezo ya kina kuhusu kupotea, kuuawa na kuteswa kwao, kwa uchunguzi zaidi.

Kesi imeahirishwa hadi Februari 22, 2023.

Chanzo: Mwananchi