Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi 3,400 za ardhi zimesikilizwa Tabora pekee

UJENZI 1 Kesi 3,400 za ardhi zimesikilizwa Tabora pekee

Sat, 8 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jumla ya mashauri 3,417 ya ardhi yamesikilizwa na Mkuu wa Wilaya ya Tabora katika kipindi cha miezi mitano iliyopita.

Akizungumza katika kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya, mkuu wa Wilaya hiyo, Dk Yahaya Nawanda amesema kati ya mashauri hayo asilimia 80 ni migogoro baina ya wanandugu.

"Asilimia themanini ya kesi za ardhi zinahusisha ndugu na ndugu jambo ambalo linaleta changamoto kubwa" amesema

Dk Nawanda amesema kila Alhamisi ambayo ameweka kuwa siku maalumu ya kusikiliza kero za ardhi, amekuwa akipokea watu kati ya 80 na 128 wanaolalamikia kuhusu mashauri ya ardhi.

Amesema anataka hadi kufikia mwezi wa nne mwaka huu, mashauri yote ya ardhi yawe yametatuliwa na kuondokana na migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Tabora.

Amebainisha kuwa changamoto za ardhi zingine zilitatuliwa na viongozi waliopita na yeye ataanza kuzitatua kwa kushirikiana na wataalamu wa ardhi na Kila wiki anatarajia kutatua mashauri 400 hadi 430 lengo ni kuimaliza ifikapo mwezi wa nne mwaka huu.

Advertisement Ametaka ushirikiano na wananchi wa Wilaya ya Tabora katika kuhakikisha hakuna migogoro mingine ya ardhi inayozalishwa katika Wilaya ya Tabora.

Mkazi wa Mtaa wa Madaraka wilayani Tabora, Yassin Hemed amesema kutatuliwa kwa migogoro ya ardhi ni jambo zuri ili watu wafanye shughuli za maendeleo.

"Kunapokuwa na migogoro ya ardhi, watu wanakosa fursa ya kufanya shughuli za maendeleo hadi tatizo litatuliwe" amesema

Mapato yapaa

Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Dk Peter Nyanja amesema Manispaa hiyo imefanikiwa kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato huku mapato ya ndani yakikadiriwa kuongezeka kutoka asilimia 76 ya mwaka 2020/21 Hadi asilimia 99.36 ya mwaka 2021/22, sawa na asilimia 23.36

Dk Nyanja amesema hilo limetokana na kuimarisha mfumo wa usimamizi wa ukusanyaji wa mapato na kuajiri watumishi wanaohusika na ukusanyaji wa mapato tu pamoja na kuimarisha kikosi kazi ndani ya halmashauri.

"Tumeongeza hali ya uaminifu na uadilifu miongoni mwa watumishi wetu" amesema

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Dk Peter Nyanja akizungumza wakati wa kikao Cha kamati ya ushauri ya Wilaya ya Tabora. Picha na Robert Kakwesi

Amesema kwa sasa wanakusanya kiwango cha juu Sh120 milioni kwa wiki wakati mwaka uliopita wa fedha walikuwa wakikusanya wastani wa Sh48 milioni kwa wiki.

Amesema wamebuni baadhi ya vyanzo vya mapato kama ujenzi wa stendi ya mabasi na malori, hosteli ya wanafunzi na ujenzi wa vibanda vya kisasa vya biashara.

Amesema kuwa wanatarajia kukusanya, kupokea na kutumia Sh44.9 bilioni katika mwaka ujao wa fedha wa 2022/23 kati ya hizo Sh5.4bilioni zikiwa ni mapato yake ya ndani.

Meya wa Manispaa ya Tabora, Ramadhan Kapela amesema kwa mwaka huu wa fedha wamepata fedha zote za maendeleo kutoka Serikali Kuu kwa asilimia mia moja.

"Tangu niwe na akili sijawahi kuona fedha za maendeleo zikitolewa kwa asilimia mia moja kama mwaka huu,mi naona ajabu" amesema

Chanzo: www.tanzaniaweb.live