Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kero ya vyoo, taa zatesa watumiaji wa Bunju Sokoni

Stendi Bunju.png Kero ya vyoo, taa zatesa watumiaji wa Bunju Sokoni

Thu, 5 Oct 2023 Chanzo: mwanachidigital

Kukosekana kwa huduma ya vyoo, taa na eneo la kuegesha magari, kuwa sehemu yenye kilima, ni miongoni mwa mambo yanayolalamikiwa na madereva, wahudumu wa magari na watumiaji wa kituo cha Bunju Sokoni, kilichopo jijini Dar es Salaam.

Kituo hicho kinatumiwa na watu wanaofanya safari zao kati ya Bagamoyo, mkoani Pwani na Dar es Salaam na Bunju Sokoni, ambapo awali kilikuwa kikitumika kituo cha Tegeta Nyuki.

Uamuzi wa magari hayo kuishia Bagamoyo uliamuliwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu (Latra) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Kinondoni, ili kulifanya soko la Bunju kupata wateja na utekelezaji wake ulianza rasmi Septemba 22, mwaka huu.

Wakizungumza madereva na wahudumu wa mabasi hayo wamesema hawaoni sababu ya mamlaka kulazimisha kutumiwa kwa kituo kisicho na miundombinu ya msingi kwa watumiaji.

Hata hivyo, Ofisa Biashara wa Kinondoni, Shedrack Mbonika alikiri kutokamilika kwa kituo hicho na akisema ujenzi bado unaendelea, hivyo kuwaomba watu wawe na subira.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, madereva hao, akiwemo Sauli Mayunga alisema stendi hiyo ipo mlimani, hivyo muda wowote magari yanaweza kuchomoka breki na kuserereka kwenda kuwagonga watu waliopo sokoni.

Alisema stendi hiyo haina choo, taa wala geti, hivyo hawawezi kufanya kazi hadi saa nne au tano usiku kwa sababu si salama kwa abiria, madereva na magari.

"Stendi hii kama unavyoiona vumbi kama lote, majani ndio kama hivyo mpaka tunakata wenyewe ili tusije kung'atwa na nyoka, kiukweli stendi hii haitufai, nadhani mamlaka ilikurupuka kutuhamishia hapa kabla ya kuimaliza," alisema Mayunga.

Heri Andrea alisema tangu waanze kuishia Bunju kipato kimepungua, kwani wakati wanaishia Tegeta Nyuki walikuwa wanatoza nauli Sh1,800, lakini kwa sasa wanavyoishia Bunju Sokoni wanatoza kati ya Sh1,200 na Sh1,300.

Andrea alisema wanashindwa kutimiza hesabu za mabosi zao ambapo kwa siku wanatakiwa kupeleka Sh80,000, badala yake hujikuta wakipata kati Sh50,000 hadi Sh60,000 kwa siku na hivyo baadhi yao mabosi wameshawanyang'anya magari.

“Uendeshaji upo juu, ikiwemo vipuri na mafuta, hivyo mabosi wanaona haiwalipi na wanapaki vyombo vyao,” alisema.

Abobakar Munisi alisema kero nyingine kubwa ni bajaji zinazopaki katika kituo hicho nazo zinaenda Bagamoyo wakiwa wanatoza Sh700 na hivyo kuwa kimbilio la abiria wengi.

"Ninavyojua bajaji kazi yake ni kuchukua abiria kutoka maeneo ya ndani kuwaleta hapa kituoni, hawafanyi kazi hiyo, badala yake nao wanafanya kama sisi na hivyo kuhatarisha maisha ya abiria pia huko barabarani," alisema Munisi.

Naye Jonathan Isimuka alisema changamoto nyingine inayowakabili ni magari mengine kutoka Bagamoyo kwenda hadi Mbezi.

"Mara ya kwanza tulipoambiwa tutakuja kuishia Bunju Sokoni, tuliambiwa TLB zote zikiisha tutaandikiwa Bagamoyo-Bunju Sokoni, lakini ajabu hapo katikati ikazuka ruti ya Bagamoyo-Mbezi.

"Hii ukifika pale stendi ya Bagamoyo inatupa wakati mgumu, kwani sisi tunaoishia Bunju tunakaa muda mrefu kupata abiria ukilinganisha na wanaokwenda kuishia Mbezi.

"Maana hakuna abiria anayeishia Tegeta Nyuki na vituo vya katikati atakuwa tayari kupanda magari mawili wakati kuna moja linaweza kumfikisha aendako," alisema Isimuka.

Latra watoa majibu

Akijibu kuhusu utoaji wa leseni za ruti, Ofisa Mfawidhi wa Latra, Mkoa wa Dar es Salaam, Rahim Kondo alisema ruti ya Bagomoyo Mbezi iliwekwa kwa ajili ya kusaidia abiria wanaosafiri kwenda mikoani.

"Tumeamua kumrahisishia abiria anayetaka kwenda mikoani, hususan kanda za nyanda za juu na kati kupanda usafiri mmoja kutoka Bagamoyo kwenda stendi Magufuli, hivyo itaendelea kuwepo.

"Huku kwa ruti ya Bagamoyo kwenda Bunju hii ni kwa ajili ya wale wanaotaka kuunga safari zao kwenda maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, ndio maana pale kituoni zipo daladala za Makumbusho, Kawe, Mwananyamala, Ubungo na pia tumeshatangaza ruti ya Kivukoni na Gerezani ambazo bado watu hawajajitokeza hadi sasa kuiomba," alisema Kondo.

Kuhusu uwepo wa bajaji, alisema wameshaanza msako wa kuzikamata juzi, na tayari wanashikilia bajaji 20 kwa kukiuka masharti ya leseni yao inayowataka kuwepo pale kwa ajili ya kukodiwa tu.

Mabasi kukacha

Mwenyekiti wa madereva hao, Salim Meru alikiri kuwapo kwa changamoto zinazopunguza ufanisi wa utoaji huduma ya usafiri.

Meru alisema ni kutokana na changamoto zilizopo na madereva kukosa hesabu, mabasi 36 kati ya 180 yameacha kufanya kazi eneo hilo.

"Hii hali ya wenetu kunyang'anywa magari inatuathiri hata kimapato chama, kwani tumekuwa tukijiendesha kutokana na michango yetu, hivyo wanachama wasipokuwa na kazi hawawezi kutoa michango," alisema Mwenyekiti huyo.

Kuhusu suala la bajaji kwenda Bagamoyo nalo alisema linawashangaza, kwani wao gari zao zikikutwa zinaenda Tanga bila kibali faini yake ni Sh250,000 na kuhoji inakuwaje bajaji hizo hazina ukomo wa safari zake.

Kutokana na changamoto hizo, Meru aliiangukia Serikali na kuiomba kuzitatua kwa kuwa walikwenda eneo hilo kwa ajili ya kutii amri za mamlaka, lakini ukweli ni kwamba mazingira hayawaridhishi.

Kuchagamsha soko

Nao uongozi wa Halmashuri ya Kinondoni, umesema moja ya sababu za magari ya Bagamoyo kuishia Bunju Sokoni ni katika kulifanya soko hilo lipate wateja.

Ofisa biashara wa Halmashauri hiyo, Shedrack Mbonika alisema soko hilo lililojengwa kwa fedha za Uviko-19 linapaswa kupata wateja, kwani bila hivyo halitaendelea.

"Ili wateja wapatikaneni lazima kuwepo na kituo kinachopakia na kushusha abiria, ambapo wengine wakisubiri kupanda gari wataweza pia kufanya manunuzi," alisema.

Hata hivyo, alisema tangu mwanzo madereva hao walionyesha nia ya kutaka kugomea kuhamia katika kituo hicho, hivyo wanachokisema hivi sasa si kigeni na kinafanyiwa kazi.

Kuhusu kuwepo kwa mwinuko kituoni hapo, Mbonika alisema wameshaweka vifusi kusawazisha na hali hivi sasa ni tofauti na ilivyokuwa huko nyuma, ambapo mvua ikinyesha kulikuwa kunaweka makorongo.

"Hata nyumba yako leo ukiijenga huwezi kuhamia ikiwa imekamilika kila kitu, kuna baadhi utamalizia ukiwa ndani tayari, hivyohivyo na kwa stendi yetu ujenzi unaendelea," alisema Shedrack.

Kuhusu vyoo, alisema hivi karibuni kitamalizika ila kinachotumika kwa sasa ni kilichopo ndani ya soko.

Wafanyabiashara, abiria wanasemaje

Kwa upande wao wafanyabiashara wamefurahishwa na uamuzi huo wa uwepo wa kituo sokoni hapo. Furahia Hussein alisema utasaidia watu walioamua kufanya biashara barabarani kwenda sokoni kuwa watakuwa na uhakika wa wateja.

Evod Lawrence, mkazi wa Bunju ambaye ni abiria alisema kwa wakazi wa Bunju na maeneo ya jirani imewapunguzia gharama za kuchukua bodaboda wanapokwenda kufanya manunuzi sokoni hapo kwa kuwa wakati magari yalipokuwa yakiishia barabarani ilibidi kukodi bodaboda.

Mina Kichawele alisema walau sasa wanaoishi Bunju watapanda kwa foleni magari hayo kwa kuwa awali walikuwa wanalazimika kupakia barabarani, tena wakati yakitoka Tegeta yakiwa yamejaza watu na wao kukosa viti vya kukaa.

Aaliya Yensen, mkazi wa Kinondoni, alisema kuzifanya gari za Bagamoyo kuishia Tegeta ni kuzidi kuongeza gharama kwa mwananchi wa kawaida ambapo badala ya kupanda gari moja anapanda mawili.

"Tulivumilia magari haya walipoyakataza kuishia Makumbusho wakayaleta Tegeta Nyuki, sasa wanazidi kuyasogeza, ipo siku yataishia Mapinga," alisema Aaliya.

Chanzo: mwanachidigital