Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Keisha awapa wosia wenzake akitoa chozi

27216 Keisha+pic TanzaniaWeb

Thu, 15 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Shinyanga. Huku akibubujikwa na machozi msanii wa muziki wa kizazi kipya, Hadija Shaaban maarufu Keisha amewataka watoto wenye ulemavu ualbino kutokata tamaa ya maisha na mazingira magumu yanayowakabili.

Akiwa ameambatana na wake wa viongozi waliotembelea kituo cha Buhangija cha Manispaa ya Shinyanga wanakolelea watoto wenye mahitaji maalumu, Keisha ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM alisema licha ya changamoto za magonjwa zinazowakabili, pia yamezuka mauaji ya kishirikina. “Magonjwa ya ngozi hatimaye saratani ni kati ya maradhi yanayowakabili wenye ualbino, hasa kutoka familia maskini zisizoweza kumudu gharama ya kununua mafuta ya kupunguza madhara ya miale ya jua mwilini,” alisema Keisha ambaye pia ana ualbino.

Wachanga Sh100 milioni

Umoja huo unaoundwa na wanawake viongozi waliopo madarakani na waliostafu, ulikichangia kituo hicho Sh100 milioni.

Licha ya mahitaji mengine, fedha hizo zitatumika kujenga na kuboresha madarasa manne na matundu manane ya vyoo kituoni hapo.

Akizungumza kituoni hapo juzi, mlezi mstaafu wa umoja huo, Tunu Pinda alisema wameamua kuchangia kiwango hicho ili kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili watoto wanaotunzwa na kulelewa hapo.

Wengine waliotembelea kituo hicho ni mke wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Germina Lukuvi, Matrida Balama ambaye ni mke wa Evance Balama aliyewahi kuwa mkuu wa wilaya mbalimbali nchini na Naima Malima, mke wa mkuu wa Mkoa wa Mara.

Katibu tawala Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela aliyeongozana na ujumbe huo alisema fedha hizo zitasaidia kuboresha mazingira wanayoishi watoto kituoni hapo na kuwaomba watu wengine wenye mapenzi mema kujitokeza kusaidia.

Naye mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Buhangija, Seleman Kipanya alisema fedha zilizochangwa na wanawake hao zitasaidia kupunguza upungufu wa madarasa na matundu ya vyoo kwa wanafunzi 1,058 wa shule hiyo, wakiwamo 230 wanaolelewa katika kituo cha Buhangija.

Shule hiyo ilikuwa na upungufu wa madarasa manane katika mahitaji halisi ya vyumba 26, huku upungufu wa matundu ya vyoo ukiwa matundu 12 kutokana shule hiyo kuwa na matundu 25 ukilinganisha na mahitaji ya matundu 37.



Chanzo: mwananchi.co.tz