Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kaya zilizoathiriwa milipuko mgodi wa Geita kulipwa bil 1.8/-

Fd883b08b3df7a62db312d4b4c3aeb10 Kaya zilizoathiriwa milipuko mgodi wa Geita kulipwa bil 1.8/-

Sat, 17 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Geita, imekamilisha kufanya tathimini ya nyumba zilizoathiriwa na ulipuaji wa miamba katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) na jumla ya kaya 1,533 zitalipwa fidia ya Sh bilioni 1.8 kutokana na athari hizo.

Mkuu wa Takukuru mkoa wa Geita, Leonidas Felix alisema hayo wakati akisoma taarifa ya kazi zilizotekelezwa na taasisi hiyo ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia Aprili hadi Juni, mwaka huu.

Alisema baada ya tathimini kukamilika, imebainika kaya hizo zenye jumla ya nyumba 2,800 zinastahili kulipwa fidia na GGML na kazi hiyo inaendelea.

Alisema hadi sasa jumla ya Sh 846,733,477 zimeshalipwa kwa wananchi wanaostahili.

Aidha, Felix alisema Takukuru imedhibiti mianya ya rushwa ya utoaji wa ajira za vibarua za ulinzi na mazingira kwenye mgodi huo na kusaidia jamii katika mitaa 25 na vijiji vitano vinavyozunguka eneo la mgodi huo kupata nafasi za ajira kwa mzunguko wa mwaka mmoja kwa kila anayepata nafasi.

Alisema pia Takukuru imekamilisha kufanya tathmini ya fidia kwa ajili ya upanuzi wa mgodi wa dhahabu wa Buckreef wenye ubia na serikali katika vijiji vya Mnekezi, Lubanda na Lwamgasa na jumla ya wananchi 851 wanaofanya shughuli zao kwenye eneo hilo watalipwa fidia ya Sh bilioni 5.7.

Mmoja ya wanufaika wa fidia ya GGML, Aroni Sabuni, mkazi wa mtaa wa Tambukareli, aliishukuru serikali kwa kusimamia kupata haki zao.

"Tunaomba zoezi hili liendelee hata sehemu nyingine ambazo hawakufika ili haki itendeke na ikiwezekana wafike kwenye vikao vya wananchi ambao hawakulipwa maana kuna wengine wameachwa kwenye tathimini," alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz