Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kaya 8,326 Tasaf kuhakikiwa upya Busega

1d725191867cf2182bc59320e8eaf545 Kaya 8,326 Tasaf kuhakikiwa upya Busega

Wed, 22 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KAYA 8,326 zilizo kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini chini ya Mfumo wa Maendeleo ya Jamii(TASAF) awamu ya tatu Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu zinatarajiwa kufanyiwa uhakiki kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa mpango huo kipindi cha pili.

Kaya hizo ni zile ambazo zilikuwa zikinufaika na mpango huo kipindi cha kwanza ambacho utekelezaji wake umekamilika ambapo uhakiki unafanyika ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Mafuguli la kuondolewa kwa kaya hewa.

Mratibu wa Tasaf wa wilaya hiyo, Wema Mrali alisema wakati wa kikao kazi cha wakuu wa idara na wawezeshaji halmashauri kilichohusu utekelezaji wa mpango huo kipindi cha pili.

Mrali alisema kazi hiyo itafanyika kwa siku tatu kuanzia leo hadi Julai 24 mwaka huu ambapo wawezeshaji hao watapita katika vijiji 46 vyenye kaya hizo kwa ajili ya kuzihakiki.

"Kwa wilaya ya Busega hakuna kaya hewa, lakini cha uhakika kwetu ni kuangalia kama kuna watu wamehama, wamefariki dunia, wagonjwa au waliingizwa kinyume cha utaratibu, yawezekana wana uwezo au ni watumishi, viongozi," alisema Mrali.

Alisema wataalamu wa kuhakiki, Kamati ya Uwezeshaji halmashuari, wamepewa mafunzo na vifaa vyote kwa ajili ya kwenda kutekeleza.

Nuru Mkomambo akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Tasaf wakati wa mafunzo kwa kamati hiyo alisema ili uhakiki ufanyike kwa ufasaha wawezeshaji hao wamekula kiapo.

Mkomambo alisema wakati Rais Magufuli akizindua kipindi cha pili cha mpango huo, aliagiza kabla ya kutekelezwa ufanyike uhakiki kaya zote kuondoa walengwa waliopoteza sifa.

Alisema Rais Magufuli alitoa agizo hilo kufuatia malalamiko mengi katika utekelezaji wa kipindi cha kwanza cha mpango huo, ikiwemo kuwepo kwa viongozi, kaya hewa, pamoja na walengwa wenye uwezo mkubwa.

Alisema kuhakikisha agizo la rais linatekelezwa, wawezeshaji wamekula kiapo kwa mwanasheria wakishindwa kutekeleza waweze kuwajibishwa.

Alisema kipindi cha pili kitatekelezwa katika halmashauri 185 Tanzania Bara na wilaya zote za Zanzibar ambapo kaya milioni 1.4 zenye jumla ya watu milioni saba watafikiwa.

Alisema kipindi cha pili cha mpango, mkazo mkubwa umewekwa kuwezesha kaya kufanya kazi kuongeza kipato pamoja na kuhakikisha huduma za jamii zinaongezwa na kuboreshwa.

Chanzo: habarileo.co.tz