Wakazi 644 wa Magomeni Kota wamegomea kusaini mkataba wa kuanza kununua nyumba hizo, kwa madai kwamba bei waliyoletewa sio rafiki na haiendani na hali ya uchumi wao.
Aidha wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati kwa kuwa bei ya Serikali iliyowasilishwa ni kati ya Sh48 milioni na Sh56 milioni ni kiwango kikubwa wanachochukulia kama mtego wa kutaka kuwafukuza.
Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa juzi na serikali kupitia kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambaye ni msimamizi wa mradi huo, mkataba huo unaanza kutumika kuanzia Februari 8 mwaka huu hivyo Kaya hizo zinapaswa kusaini kwa bei waliyoletewa.
Mwanasheria wa wakazi hao, Twaha Taslima akisoma barua iliyoandikwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Daud Kandoro, kwenda kwa wakazi hao, jana siku ambayo walifanya kikao mkoani Dar es Salaam, alisema bei iliyowasilishwa na serikali awali ilikuwa ndogo.
“Bei ambayo ilipendekezwa na Serikali awali ilikuwa ni Sh12 milioni hadi Sh17 milioni, iliyotolewa Juni mwaka jana, haikukidhi thamani ya eneo, haikujumuisha faida wala huduma za maeneo yanayozunguka makazi hayo ambayo ni jumuishi,” amesema.
Taslima amesema, "Njia mojawapo ya kuchukua ni kuiomba Serikali au kwenda mahakamani. Bei ya chumba na sebule kwa Sh48. 5 milioni na vyumba viwili na sebule Sh56.8 milioni inaweza isiwe rafiki na mnunuzu asimudu," alisema Taslima.
Mwenyekiti wa Wakazi wa Magoneni Koti, George Abel, amesema kwamba bei zilizokokotolewa siyo rafiki kwa wakazi hao, licha ya Serikali kuongezewa mkataba wa kulipa na kuishi kutoka miaka 10 hadi 15.
Amesema kuwa bei hiyo inatakiwa kila mkazi alipie Sh300,000 kwa mwezi hivyo kwa mwaka ni Sh3.6 milioni akisema kiasi hicho ni kikubwa ikizingatiwa baadhi ya wakazi tayari ni wazee na wastaafu.
"Tumepokea barua hii ikiwa zimebaki siku tatu tu kwamba tusaini mkataba wa manunuzi, tukutane tujadiliane kabla ya tarehe 8, Februari, mwaka huu, hizi bei si rafiki haziendani na hali za wakazi walio wengi," amesema Abel.
Mmoja wa wakazi wa nyumba hizo, Salama Goronga (65), amesema barua hiyo iliyosomwa kwao, ikionyesha bei hiyo imewahuzunisha kwa kuwa haiendani na hali zao kimaisha.
"Mimi nina wajukuu, na iliposomwa barua machozi tu yameanza kunitoka hiyo pesa nitatoa wapi, nitaondoka hapa niende wapi," amesema Salama.
Mkazi mwingine, Mwajuma Hamisi (82), amesema ana watoto wawili wa walioolewa ndio wanaomtunza kwa kumnunulia chakula na mahitaji mengine, hivyo itawawia vigumu leo hii waanze kumtafutia kodi mara atakapoondoka kwenye makazi hayo kutokana na kushindwa kulipia.
"TBA wanaotaka hizo nyumba, leo bei hii, kesho hii, tutalipaje mimi mzee, wanitoe hapa si aibu kwangu, mamilioni hayo nitayatoa wapi," amesema Mwajuma.
Alipoulizwa Kaimu Mkurugenzi kutoka idara ya miliki TBA, Said Mndeme amesema “Masuala hayo aulizwe mkuu wa taasisi ndiye anayejua,” amesema