Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kaya 500 zajiandikisha kuhama Ngorongoro

Ngorongoro 71056561 Kaya 500 zajiandikisha kuhama Ngorongoro

Fri, 5 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Awamu ya pili ya zoezi la uhamaji kwa hiari kwa wananchi wanaoishi ndani ya eneo la hifadhi ya Ngorongoro jijini Arusha, imeanza rasmi kwa kaya 30 zenye watu 224 na mifugo 393 kuhamia rasmi kwenye maeneo yaliyotengwa na Serikali kijijini Msomera mkoani Tanga. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Hayo yamebainishwa leo tarehe 5 Januari 2024 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, akitoa taarifa ya maendeleo ya zoezi hilo, jijini Dar es Salaam.

“Zoezi hili linaendelea vema ambapo leo Ijumaa, kundi la kaya 30 linahamia kijijini Msomera. Hili ni kundi la kwanza katika awamu ya pili la wananchi wanaohamia Msomera. Kundi hili linakwenda kuungana na wananchi wengine 3,010, kutoka kwenye kaya 551 zenye mifugo 25,521 ambao walihamia kwenye awamu ya kwanza baada ya nyumba 503 kukamilika kijijini Msomera,” amesema Matinyi.

Msemaji huyo wa Serikali amesema, hadi kufikia tarehe 31 Disemba 2023, ujenzi wa nyumba 350 umekamilika Msomera na kwamba zoezi la wanaotoka Ngorongoro kuhamia kijijini hapo litaendelea ndani ya Januai 2024.

Amesema, tayari kaya 500 zimejiandikisha kuhama kwa hiari hifadhini hapo, ambapo 406 zimeshafanyiwa tathmini ya malipo yao ya fidia na ya ziada.

Mbali na kundi hilo linaloekea Msomera, Matinyi amesema kundi jingine la kaya 25 zenye watu 172 na mifugo 213 linahamia maeneo mengine ya nchi ambayo ni ya mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Simiyu na Tanga.

“Serikali inaendelea kusisitiza kwamba zoezi hili ni la hiari kwa sababu kuu mbili: Moja, ni kuwahamishia wananchi wa Ngorongoro kwenye eneo bora kwa  ajili ya maendeleo yao ya huduma za kijamii pamoja na usalama wao. Pili, ni kuendeleza na kutunza uhifadhi wa eneo la Ngorongoro ambalo linaheshimika kimataifa kama moja ya maeneo ya urithi wa dunia,” amesema Matinyi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live