Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kaya 50 zazingirwa na maji Bukoba

Mafuriko Bukoba DSC07455 Kaya 50 zazingirwa na maji Bukoba

Thu, 18 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kaya 50 zimekosa makazi baada ya kuzingirwa na maji katika Mtaa wa Kyaya Kata Kahororo Manispaa ya Bukoba kutokana na mvua kubwa iliyonyesha Aprili 12, 2024.

Kwa sasa kaya nane kati ya hizo zilizoathiriwa na maji ya mvua zimepewa hifadhi katika Kituo cha Afya Kashai huku nyingine 42 zikiikataa hifadhi hiyo ya muda.

Akizungumza jana Aprili 17, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima amesema kamati ya usalama ya wilaya imetembelea maeneo yaliyozingirwa maji.

Sima amesema kata zimeathiriwa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kusababisha mkondo wa maji ya Ziwa Victoria kumwaga katika makazi yao.

Amesema Serikali inaendelea kuweka utaratibu kuhakikisha watu wote waliopo kwenye maeneo yaliyozingirwa maji wanahamishwa na kutafutiwa hifadhi.

“Mpaka sasa tunaendelea na utaratibu wa takwimu ili kubaini ni watu wangapi wanaishi mtaa huo na nyumba zilikuwa ngapi, ila kule katika Kituo cha Afya Kashai kaya nane tayari tumeziweka zenye watu 30 wanawake wapo saba, wanaume watano na watoto 18 hivyo, tunahimiza wananchi kuhama kwenye maeneo hayo yanayoendelea kuathiriwa,” amesema Sima.

Ananastella Longtone mmoja wa waliopewa hifadhi amesema Aprili 12, 2024 saa 9:30 usiku mvua ilianza kunyesha taratibu hadi ilipofika saa nne asubuhi, maji yalianza kuingia ndani ya nyumba yake na kuzingira kila kitu.

Amesema ilimlazimu yeye na familia yake kutafuta kichuguu (sehemu iliyoinuka), walikaa hapo hadi saa tisa mchana mvua ilipokatika.

"Mvua ilinyeshaa usiku kucha mimi, mume wangu na watoto tukazidiwa, mida ya saa nne asubuhi tulitoka bila kitu ndani hadi kwenye kichuguu kilichopo hapo nyumbani tulichokuwa tunakitumia kuanikia dagaa… tumekaa mpaka mvua ilipokata na baadaye tukatoka mpaka ofisi za kata,"amesema Annastella.

"Maji yamejaa kwenye nyumba, vitu vyetu vimeharibika hatuna chochote ila tunashukuru kwa misaada tunayozidi kupokea.”

Marco Projestus (15), mwanafunzi wa kidato cha pili Shule ya Sekondari Kashai ameshukuru viongozi mbalimbali wanaoendelea kufika katika kituo hicho na kuwapa misaada ya mahitaji ya shule.

Mbunge wa Bukoba Mjini, Stephen Byabato ametoa msaada wa majiko ya gesi kwa waathirika hao ambao katibu wake, Pasaka Kiraka ameukabidhi kwa niaba yake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live