Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kauli za viongozi Serikali zinavyowagharimu wakazi 1,860 wa Kipunguni

FFSDtSpg.jpeg Kauli za viongozi Serikali zinavyowagharimu wakazi 1,860 wa Kipunguni

Mon, 8 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Danadana na kauli za viongozi wa Serikali zimeendelea kuwagharimu wakazi 1,860 wa Mtaa wa Kipunguni A kwa kutowalipa fidia ya nyumba na maeneo yao baada ya kuyafanyia tathimini ili wahame kupisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Hali hiyo imeendelea kuwa shubiri kwa wakazi hao ambao wengi wao ni wastaafu wa ngazi mbalimbali serikalini kiasi cha kubaki njia panda wakishindwa kufanya shughuli zozote za kiuchumi na maendeleo katika maeneo hayo huku nyumba zao zikiendelea kuwa maghofu.

Sakata hilo lilianza miaka 28 iliyopita baada ya Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (Taa) kuja na mpango wa kupanua uwanja huo, ambapo jumla ya wakazi 1,860 wa walifanyiwa tathimini ya nyumba na mali zao zingine.

Katika eneo hilo, tathimini imefanyika mara mbili, ya kwanza ilifanyika miaka 28 iliyopita ambayo hakuna mwananchi aliyelipwa licha ya kila mkazi kujulishwa anatakiwa kutoliendeleza eneo lake kwa kuwa anatakiwa kuhama.

Julai 2022, Serikali ilifanya marejeo ya tathmini kwa wakazi hao na iliridhia kuwalipa Sh147 bilioni lakini hadi sasa wamekuwa wakipigwa danadana.

Julai 2023, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alitembelea eneo hilo na kufanya mkutano wa hadhara ambapo aliahidi watalipwa kabla ya Septemba 2023.

Katika mkutano huo, Dk Nchemba aliambatana na Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu na Mbunge wa Segerea (CCM), Bonnah Kamoli huku wote wakiwatoa wasiwasi wananchi hao kwamba Serikali ina fedha na wasubiri malipo ili wahame lakini hadi sasa bado.

Mwananchi baada ya kumtafuta Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi kujua kilichokwamisha malipo ya wananchi hao, Matinyi amesema anafuatilia kujua changamoto hiyo lakini akasema atafutwe Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (Taa), Mussa Mbura kwa majibu.

Alipotafutwa Mbura amesema Serikali bado inalifanyia kazi jambo hilo na kuwa wananchi walijulishwa wakitakiwa kuwa wavimilivu na watulivu wakati taratibu za kuwalipa zikielendelea.

“Ni kweli imechukua muda mrefu lakini Serikali ina nia kweli ya kuwalipa na kumaliza hilo jambo, ndiyo maana tukafanya tathmini na wananchi wana taarifa kamili,” amesema.

Mbura amesema ugumu unaotokea kwa sasa ni kwa sababu Serikali inaandaa utaratibu wake wa ndani ili kuhakikisha fedha hizo zinapatikana na wananchi wanalipwa.

“Muda wowote kuanzia sasa watalipwa fedha zao, najua hawana shida ya kuhama kwa kuwa tulijitahidi kuwapa elimu ya kutosha na nia ya Serikali ni kuwalipa kwa hiyo ni jambo la muda sana,” amesema,

Amesema walitamani kuwalipa hata kesho au leo ili wakaendelee na maisha maeneo mengine.

Malalamiko ya wananchi

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao wamesema kama Serikali haina mpango na eneo hilo ni muhimu ikawaeleza ili wawe huru kufanya shughuli za kimaendeleo.

“Tangu mwaka 1997 tulifanyiwa tathmini ya kwanza lakini hakuna chochote kilichotokea na mwaka 2022 walirudia tena kufanya tathmini na kuahidi itakuwa ni mara ya mwisho na watatulipa fidia kwa muda uliopangwa,” amesema Mdamiru Salim.

Amesema hali hiyo pamoja na kauli zinazotolewa na viongozi zinafanya maisha yao kuwa magumu kutokana na makubaliano waliyoingia kufanyana shughuli zozote za maendeleo kama kufuga au kulima.

“Maisha ya Kipunguni yamekuwa magumu sana, nyumba zinabomoka tunashindwa kutengeneza, vyoo vinabomoka, tunahisi kama Serikali imetutenga na kutunyanyasa,“ amesema Salim

Naye Pentavalina Malumu ambaye ni askari polisi mstaafu, ameiomba Serikali kuwaangalia kwa kuwa yeye umri wake umeenda na baada ya kustaafu aliwekeza kwa kujenga nyumba ili kupata mahitaji yake kupitia kodi anayokusanya.

“Kwa sasa wapangaji kwa asilimia 90 wameondoka na waliobaki hawalipi kodi kwa wakati na wengine hawatoi kabisa, kutokana na ugumu wa maisha wa eneo hilo, ukiwafuata wanakukatalia,” amesema.

Amesema ana eneo kubwa katika mtaa huo alikuwa analima na kufuga kuku lakini baada ya kupewa waraka wa kutakiwa kuhama ameshindwa kuendeleza shughuli zake za kujiingizia kipato.

“Nimeshindwa kuweka kuku wa kunisaidia katika maisha yangu, tunachoomba ni kupata fedha zetu tukaanze maisha mapya sehemu zingine,” amesema Malumu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live