Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kauli za uvumilivu zatawala mazishi ya mama yake Sugu

Thu, 30 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Unaweza kusema kauli za kusisitiza amani, upendo na uvumilivu vilitawala maziko ya Desderia Mbilinyi, mama mzazi wa mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph maarufu Sugu yaliyofanyika jana jioni mjini hapa.

Viongozi mbalimbali walioshiriki misa ya mazishi ya Desderia aliyefariki Agosti 26 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa akipatiwa matibabu, Freeman Mbowe na naibu spika, Dk Tulia Ackson walisisitiza amani, upendo na uvumilivu miongoni mwa watu.

Akizungumza nyumbani kwa Desderia eneo la Sai jijini hapa, Mbowe aliwataka wanachama wa Chadema na wapenda haki kuwa imara licha ya kuwa kwa sasa upinzani unapita katika kipindi kigumu na kukumbwa na misukosuko.

Alisema taifa linapitia katika majaribu na kukabiliana nayo kunahitaji umoja na mshikamano wa dhati kwa Watanzania wote, wakiwamo wa CCM na wapinzani.

“Kama kuna kipindi ambacho Watanzania wanahitaji umoja ni hiki, wale wenye roho nyepesi wanakimbia, waache wakimbie tutabaki wachache ambao tutakomaa,” alisema Mbowe.

Pia, baada ya misa ya mazishi, Mbowe alisema kwa sasa kuna uhasama wa kisiasa jambo alilobainisha kuwa si jema kwa taifa.

“Kama hatuwezi kushirikiana katika maisha ya kawaida, kama hatuwezi kushirikiana masuala ya kijamii na hatuwezi kuheshimiana katika uongozi ambao tumepewa na watu, utakuwa ni unafiki kushirikiana katika misiba haya madaraka yanapita,” alisema.

Alimshukuru mkuu wa wilaya ya Mbeya, William Ntinika, kwa maneno yake ya faraja licha ya mkuu wa mkoa huo mara kadhaa kubeza uwapo wa Chadema mkoani Mbeya.

Naye Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye aliwashukuru wananchi wa Mbeya kwa kushiriki katika msiba huo bila kujali itikadi zao, kuwa tofauti na maeneo mengine ambayo upande mmoja hususia kushiriki misiba.

Sumaye aliwataka wenye tabia za kususia misiba kuacha tabia hiyo italipeleka Taifa pabaya.

Akitoa shukurani zake, Sugu aliwashukuru wote waliompa pole na kumtia moyo kufuatia msiba huo wakiwamo madaktari ambao walijitahidi kuokoa maisha ya mama yake huku akimtaja Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwa alimpigia simu kumpa pole.

Akitoa salamu za wabunge wa Mbeya, Dk Tulia alisema: “Watu wa Mbeya ni jambo jema kushirikiana katika kila jambo. Sugu ni kaka yangu, hivyo tunatoa rambirambi lakini mimi kwa vile nimefika ninatoa rambirambi yangu.”

Naye katibu wa uenezi wa CCM Mbeya, Bashiru Madodi alisema: “Tumekuja hapa kwa ajili ya msiba wa mama yetu, mama yako Sugu ni mama yetu. Tukiwa kwenye siasa tutashindana, yanapokuja matukio muhimu na makubwa kama haya ni wajibu kushirikiana na kulia pamoja.”

Chanzo: mwananchi.co.tz