Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kauli ya RC Hapi kuhusu Hilda wa Chadema yamuibua Zitto, Mchungaji Msigwa

Fri, 21 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wito uliotolewa katika mitandao ya kijamii na mtu aliyejitaja kuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi kwa mwanachama wa Chadema, Hilda Newton umeibua mjadala kwa watu mbalimbali ‘kumshambulia.’

Hatua hiyo inatokana na jinsi mtu huyo aliyejitambulisha kwa jina la Hapi alivyotumia katika ukurasa wa Twitter kumtaka Hilda kujisalimisha kwa mkuu wa polisi mkoa wa Iringa, Juma Bwire leo Ijumaa Desemba 21, 2018 saa 2 asubuhi.

Kupitia ukurasa huo wa Twitter, uliandikwa wito huo jana Alhamisi Desemba 20, 2018 huku ikiwa imeambatanishwa picha ya Hilda aliyepiga na rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume.

“?Mlio karibu na huyu binti mfupi wa Bavicha mkumbusheni kesho tarehe 21 saa 2 asb ndio mwisho wa kujisalimisha kwa hiyari kwa RPC Bwire Central Police Iringa,” ulisomeka ujumbe huo.

Watu mbalimbali wamechangia ujumbe huo na miongoni mwao ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akisema, “Kwanini unakosa busara? Unamwita mtu mfupi? Halafu wewe ni Kiongozi? Huna mamlaka ya kumwita mtu yeyote kuripoti Polisi.”

“Hatakuja na hutafanya kitu. Jifunze hekima za uongozi Ally. Usiwe na kibri kwani kibri si maungwana. Sasa Hilda hatatii amri yako batili. Tuone utafanya nini,” ameandika Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini

Zitto ameungwa mkono na mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche akisema, “Mtume Bwire amtafute, hatajisalimisha unless useme sheria gani inakupa mamlaka wewe kumsummon!!! Tumia madarakani vizuri bado wewe ni kijana, lakini kwa sababu yamekulevya hautaelewa.”

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa naye amechangia ujumbe huo akisema, “Hayo ni matumizi mabaya ya madaraka! Uongozi wa kutisha tisha watu umepitwa na wakati, kama umekosewa fuata taratibu za kisheria, huna madaraka ya kukamata kamata watu ovyo!”

Kwa upande wake, Abdallah Komba naye amechangia ujumbe huo wa Hapi kwa kusema, “Mwenyezi Mungu ametuumba kwa maumbo na rangi tofauti ili tupate kujuana na aliye bora katika hao ni mwenye kumcha Allah. Hapi wewe unakosoa uumbaji wa Mola wako kwa ulevi wa madaraka?”

Soma Zaidi: Hilda wa Chadema amgomea RC Hapi

 



Chanzo: mwananchi.co.tz