Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kauli ya Muliro yazua mjadala

Mulirooo Kauli ya Muliro yazua mjadala

Fri, 17 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kauli ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi (ACP) Jumanne Muliro, kwamba raia anaruhusiwa kuomba lifti kwenye gari la polisi, imeibua mjadala huku baadhi wakionyesha hofu ya kubambikwa kesi.

Jumanne ya wiki hii, Kamanda Muliro wakati akihojiwa katika kipindi cha Clouds360 cha Clouds TV, alisema kwa nini mtu asilisimamishe gari la polisi na kuomba lifti.

“Kuna mtu alishawahi kuomba lifti kwenye Defender (gali la polisi) hakupewa? Kwa nini wanapanda watuhumiwa tu? Kwa mfano Defender linakwenda Bunju, Tegeta, Kunduchi, Kitunda au Mwanagati, Kivule analiona kabisa limeandikwa Polisi na wewe unakwenda maeneo hayo kwa nini usilisimamishe ukaomba lift?” alihoji Kamanda Muliro.

Baadhi ya wananchi, wakitoa maoni kuhusu kauli hiyo, walisema kuliko waombe lifti kwenye gari la polisi ni bora waendelee kutembea.

Katika mtandao wa Instagram, Hamisi Mussa aliandika kuwa: “Hawana noma, kweli mimi nimeshapanda toka Mabwepande mpaka Tegeta, kwanza na stori tunapiga vizuri tu.”

Amedeus Kiwango aliandika: “Yaani ni bora nikatembea kama ni msituni nikaliwa na Simba kuliko kuomba lifti humo.” Mchangiaji mwingine anayejiita Madam ZP aliweka emoji ya kucheka na kuandika, “dah hapana nitatembea tu.”

Mchangiaji anayejiita Pi_Tanzania_Official kwa upande wake aliandika, “Naijua iyoo (hiyo) unaingia tu wanakuambia utaenda kutusaidia upelelezi wa ‘panya road,” huku Mutta_Ab akiandika kuwa, “Watu wenyewe wanakuangalia kama vile ni washirikina utaanzia wapi?”

WADAU WAFAFANUA

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, akizungumza na Nipashe kuhusu kauli hiyo, alisema si sahihi raia kuomba lifti kwenye magari hayo.

“Si sahihi hata kidogo. Ninadhani aliongea kama kufurahisha umma au kujifurahisha. Gari  la polisi ni kama magari ya watumishi wa umma, huwezi kuomba lifti gari la waziri au magereza.

"Huo si utaratibu, likitokea tatizo lolote la kibima sheria inakataza kabisa kumpa mtu lifti au kumpandisha mtu ambaye hahusiki,” alisema huku akibainisha kuwa magari ya polisi hayana bima kwenye kampuni binafsi, hivyo ikitokea ajali yoyote itakuwa ngumu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live