Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Katibu Mkuu asifu kituo kwa kunenepesha mbuzi 1,472

1517399aa27ba3b658952807a22e1894 Katibu Mkuu asifu kituo kwa kunenepesha mbuzi 1,472

Sun, 19 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo), Profesa Elisante Ole Gabriel (pichani) amepongeza Kituo cha Ubunifu wa Kilimobiashara (AIC) cha PASS-Trust, ambacho ndani ya miaka miwili kimenenepesha mbuzi 1,472 na kuwauza kwa bei ya faida.

Akizungumza katika Ofisi za Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), alisema Pass imepasi mtihani kwa kuanzisha kituo atamizi, ambacho tayari kimeelimisha vijana 27 kwa kuwapa taaluma ya namna ya kunenepesha mbuzi na kuwauza baada ya kuongeza thamani. Profesa Gabriel alisema Pass imekuwa ikisaidia vijana kunenepesha mbuzi, kufuga, kuchinja na kuuza nyama, bila kujali kiwango cha elimu yao.

Katika kufanyia mazoezi elimu hiyo, vijana hao wanajua kufuga, watachinja na kuuza nyama ya mbuzi kwa wasafiri wanaotumia barabara ya Morogoro. Alitoa wito kwa wahitimu wote wa ngazi yoyote, kuacha mtindo wa kungoja kuajiriwa, badala yake kutumia elimu yao kuanzisha shughuli mbalimbali katika sekta ya mifugo na nyingine ili kusaidia wengine kuajiriwa.

Alimuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Dk Omari Nkulo kusaidia vijana hao kujiajiri na kuwapa mikopo kupitia mapato ya ndani ya asilimia nne ili kuanzisha vituo kama hicho katika maeneo mbalimbali ili kusaidia wengine.

Ofisa Maendeleo ya Biashara wa Kituo hicho, Eva Idd alisema kuwa kituo hicho kilianzishwa 2018 na wahitimu wa kwanza walitoka mwaka uliofuata. Hadi sasa vijana 27 wamepata mafunzo ya kunenepesha mbuzi 1,472 walionunuliwa vijijini na kuwauza kwa faida.

Eva alisema kituo hicho kilichoanzisha kwa ushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), kimepata mafanikio makubwa kwa kuwaelimisha vijana hao 27 namna ya kunenepesha mbuzi na kinalenga kuwafikia vijana 50 ifikapo 2021.

Alisema kituo hicho atamizi kipo eneo la Mbande wilayani Kongwa katika barabara ya Morogoro. Kimekuwa msaada mkubwa kwa vijana katika kuwafunza biashara ya mifugo hasa mbuzi, kwa kuwanenepesha ili kuongeza thamani na kuwauza au kuchinja nyama.

Eva alisema kwa mwaka huu, kituo hicho kina vijana saba ambao wanapata mafunzo, ujuzi na weledi wa kunenepesha mbuzi na wakihitimu wanapanga kwenda kuanzisha huduma kama hizo katika vijiji vyao.

Vijana wanapokuwa katika kituo hicho atamizi, pia wanajifunza, ufundi wa kutengeneza mabanda bora ya mbuzi, kuangalia afya ya mbuzi, jinsi ya kunenepesha na usimamizi wa mbuzi kwa ujumla.

Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, Dk Eligy Shirima alisema taasisi yake inashirikiana na Pass kwa kuwapa eneo na kuwaelimisha vijana kunenepesha mbuzi na kufanya utafiti wa namna bora ya kufuga mifugo hiyo katika maeneo mbalimbali.

Chanzo: habarileo.co.tz