Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Katibu Mkuu aagiza kisima kirefu Mpandangindo

714ce75d4f73bf08bbfd332df217febf Katibu Mkuu aagiza kisima kirefu Mpandangindo

Wed, 2 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji, Anthony Sanga, ameiagiza Wakala wa Maji Vijijini (Ruwasa) kupeleka mashine ya kuchimba visima vya maji katika kijiji cha Mpandangindo kwa ajili ya kutatua kero ya muda mrefu ya maji safi na salama kwa wakazi wa vijiji vitatu vya Mpandangindo, Liweta na Kituro.

Sanga alitoa agizo hilo jana katika kijiji cha Mpandangindo Jimbo la Peramiho halmashauri ya wilaya Songea mkoani Ruvuma, baada ya kupata taarifa ya kero ya maji na maombi ya kuchimbiwa visima kutokana na changamoto kubwa ya maji inayowakabili wakazi wa kijiji hicho.

Alisema alipata habari kupitia mbunge wa jimbo la Peramiho, Jenista Mhagama juu ya shida ya maji katika jimbo hilo ndiyo maana amefika ili kujionea mwenyewe kuhusu kero hiyo ya maji kwa wananchi.

Aidha, aliagiza kuanzia wiki ijayo timu ya wataalamu kufika katika eneo hilo ili kuangalia na kufanya utafiti ni eneo gani lenye maji mengi ambalo litafaa kwa ajili ya kuchimba kisima cha maji.

Alisema fedha kwa ajili ya kazi hiyo zipo na kinachosubiriwa na wataalamu wa wizara hiyo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Peramiho Jenista Mhagama alisema jimbo hilo lina miradi ya visima virefu 39 katika vijiji 20, lakini hadi sasa ni visima 19 vilivyochimbwa.

Mhagama aliiomba serikali kutafuta njia ya kumaliza tatizo la maji katika vijiji vilivyobaki ili wananchi waondokane na kero ya kuamka usiku wa manane kwenda kutafuta maji.

Mmoja wa wakazi wa kijiji cha Mpandangindo, Generosa Fussi alisema kwa sasa wanapata huduma ya maji kutoka kwenye visima vichache vilivyochimbwa na taasisi moja, hata hivyo maji hayo bado hayatoshelezi kutokana na idadi ya wananchi waliopo katika kijiji hicho.

Chanzo: habarileo.co.tz