Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kasi ndogo ya mkandarasi yamkera Kusaya

6ce983909071965cbf764d5719510d4d.jpeg Kasi ndogo ya mkandarasi yamkera Kusaya

Fri, 18 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KATIBU Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya amesema atachukua hatua kali dhidi ya mkandarasi Bogeta Engineering Co. Ltd kwa kutekeleza ujenzi wa ofisi na hosteli katika chuo kwa kasi ndogo na kiwango duni cha ubora.

Alisema hayo juzi alipofanya ziara ya kushitukiza katika Chuo cha Mafunzo ya Kilimo (MATI)-Mubondo wilayani Kasulu akiwa njiani kwenda Kigoma kwa ziara ya kikazi.

Katika ziara hiyo ya kushitukiza, Kusaya alishuhudia mafundi wakiendelea na kazi, lakini kwa kasi ndogo huku kukiwa na upungufu mkubwa katika ubora wa kazi.

“Sijaridhishwa na kasi ndogo ikiwemo ubora wa kazi hususani upande wa marumaru; kuna upungufu mkubwa wa ubora, hivyo mwambieni mkandarasi afanye maboresho ya kazi na ifikapo Januari 15, mwakani nahitaji anikabidhi kazi ikiwa na ubora uliokusudiwa kwa mujibu wa mkataba,” alisema Kusaya.

Aliagiza mafundi wa kampuni ya Bogeta kuondoa kasoro zikiwemo marumaru kupishana, miundombinu ya umeme kutowekwa vizuri na pia, kukamilisha upakaji rangi katika majengo hayo ili ifikapo Januari mwakani yawe yamekamilika na kuanza kutumika.

Mkuu wa Chuo hicho, Mubondo Nzully, alisema mradi huo wa ukarabati wa ofisi ya utawala na bweni la wanafunzi ulianza Mei mwaka jana ukitarajiwa kukamilika ndani ya siku 60.

Kwa mujibu wa Nzully, mradi huo umegharimu Sh milioni 367.3 na ukikamilika, utasaidia kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi na kuongeza nafasi ya wanafunzi kuishi chuoni hapo wakati wa mafunzo yao.

Chanzo: habarileo.co.tz