Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kasesela amjia juu Msigwa

20684 Kasesera+pic TanzaniaWeb

Thu, 4 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Iringa. Mkuu wa  Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela amemjia juu Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Peter Msigwa kwa kubeza ziara ya mkuu wa mkuu wa mkoa huo, Ally Hapi.

Hapi alifanya ziara hivi karibuni katika tarafa 15 za mkoa huo akiwa na waandishi wa habari, ziara iliyokuwa na kauli mbiu ya Iringa Mpya.

Ziara hiyo ilimwezesha mkuu huyo wa mkoa kupokea na kuzitafutia majibu zaidi ya kero 800 za wananchi na kumfikisha katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayofanywa na Serikali kwa ushirika na wadau wake.

Hapi anasema dhana ya ujenzi wa Iringa Mpya inalenga kuwatoa maofisini watendaji wa Serikali, kuamsha ari yao ya utendaji na kuwapeleka kwa wananchi kusikiliza kero zao, kuzifanyia kazi na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mbunge wa Iringa Mjini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa anasema dhana hiyo ina mapungufu kwa kuwa haikuwa shirikishi na ililenga kumjenga na kumuongezea umaarufu mkuu huyo wa mkoa.

“Dhana ya Iringa mpya si shirikishi na haieleweki wadau wake ni akina nani, kama ni CCM, mkuu wa mkoa mwenyewe, UVCCM, mabaraza ya madiwani au wananchi wote?”Anahoji  Msigwa

Amesema  akiwa Iringa Mjini, Hapi alitumia madaraka yake vibaya kwa kuagiza mtumishi mmoja kusimamishwa kazi, mwingine kushushwa cheo au kuondolewa katika kituo chake cha kazi na akaamuru diwani wa viti maalumu na kaimu meneja wa Tanesco Iringa kuwekwa rumande kwa saa tofauti kabla hajabatilisha agizo hilo kwa ofisa huyo wa Tanesco.

Akimtishia kumburuza mahakamani mkuu wa mkoa huyo,  Msigwa amehoji ukubwa wa msafara na kiasi cha fedha zilizotumika katika ziara ya kiongozi huyo katika mazingira aliyosema idara nyingi za Serikali zinalalamika kukosa fedha za kusimamia utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe (Chadema) amesema zaidi ya Sh 40 milioni zimetumiwa na manispaa hiyo kulipa waandishi, mafuta ya magari, matangazo na mapambo katika ziara ya siku nne iliyofanywa na mkuu wa mkoa huyo katika halmashauri hiyo.

Kimbe amesema watahitaji ufafanuzi kutoka kwa watendaji wa halmashauri hiyo kujua fedha hizo zilikotolewa na kufanyiwa matumizi hayo bila ridhaa ya vikao halali vya halmashauri.

Kwa upande wake Kasesela, amewataka wananchi kumpuuza Msigwa akisema haiwezekani mbunge huyo akazuia kitu kinacholeta maendeleo na kwamba  mkuu wa mkoa au kiongozi mwingine yeyote hahitaji kibali au ridhaa ya watu wengine kusikiliza kero za wananchi.

“Kero nyingi za wananchi ni kero ambazo zilipaswa kusikilizwa na Msigwa, badala yake yeye amekuwa mtu wa kuzungumza tu mambo ya kitaifa kwenye vyombo vya habari, hakutani na wananchi wake na kusikiliza kero zao labda kwa kuwa anaogopa akidhani kila mwananchi anayemtafuta anataka kumuomba hela.”

Akizungumzia msafara mkubwa katika ziara hiyo, Kasesela amesema kazi kubwa ya magari ya Serikali ni kuwawezesha  kuwafikia wananchi kwa urahisi na kushughulikia changamoto zao.

“Waliopewa magari hayo wanaweza kuwafikia wananchi wakiwa kama timu au mmoja mmoja kwa kuzingatia mazingira ya wakati huo. Mkuu wa Mkoa alitaka aambatane na watendaji katika ziara yake ili wananchi wapate majibu ya kero zao mbele yake, kwa hiyo hilo si kosa,” amesema.

Kuhusu adhabu zilizotolewa kwa baadhi ya watendaji, Kasesela  amesema: “Kinachinishtua ni mheshimiwa huyo kuwa mtetezi wa watumishi wabovu. Msigwa ni mbunge wa wananchi, waliowalalamikia wananchi, walioadhibiwa ni wananchi wapiga kura wake. Inakuwaje awatetee watumishi wanaolalamikiwa na wananchi wake?”

Kasesela amemtaka Msigwa kujiunga na vyama vya wafanyakazi kama amechoka siasa, kwani huko ndiko mahali mwafaka ambako wafanyakazi wanaweza kutetewa kutokana na makosa yao ya kiutendaji.

Wakati huohuo Kasesela amemshutumu mbunge huyo na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Alex kwa kutumia ofisi ya meya kufanya shughuli zao za kisiasa.

Amesema mbunge na meya huyo wanapokuwa na shughuli zao za kisiasa wanatakiwa kuzifanya nje ya ofisi hiyo inayohudumia wananchi wote bila kujali itikadi zao za kisiasa.

Pamoja na shutuma hiyo, amesema ni makosa kwa meya huyo kutumia gari la meya kwa shughuli zake binafsi na kwa zaidi ya siku mbili anazotakiwa kwa mujibu wa taratibu bila taarifa yoyote.

“Meya anatakiwa kuwepo ofisini siku ya Jumanne na Alhamisi tu, na anatakiwa kutumia gari la Serikali katika siku hizo na pale anapokuwa na shughuli za kiserikali. Tutaanza kumfuatilia na tutamzuia kutumia gari hilo kwa mambo yake binafsi,” amesema.

Kasesela amesema madai ya Mstahiki Meya kwamba ziara ya mkuu wa mkoa katika halmashauri hiyo imetumia zaidi ya Sh 40 milioni hayana ukweli wowote na anachojua yeye ni kwamba sehemu kubwa ya fedha zilizotumika zilichangwa na marafiki wa Hapi na wadau wengine walioombwa kusaidia.

 

Mchungaji Msigwa kumfikisha RC Hapi mahakamani

Chanzo: mwananchi.co.tz