Mahakama Kuu ya Tanzania imewaamuru wananchi 233 wa kijiji cha Selekano Kata ya Liganga katika Wilaya ya Songea, kuondoka katika eneo lenye ukubwa wa hekari 1,160, ikisema ni mali ya Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Songea.
Hukumu hiyo inayotokana na kesi ya ardhi namba 5 ya mwaka 2021 iliyofunguliwa na Saulo Sanga na wenzake 232 dhidi ya Baraza la Wadhamini wa Kanisa Katoliki Jimbo la Songea, imetolewa Alhamisi ya Machi 21, 2024 na Jaji James Karayemaha.
Katika hukumu yake hiyo, Jaji aliyakataa maombi ya wananchi hao na kutamka wao ndio wavamizi wa eneo hilo na wametakiwa kuondoka, huku pia akiyatupa maombi yao ya kutaka Mahakama itamke wao ndio wamiliki halali.
Pamoja na maombi hayo, wananchi walikuwa wanaiomba Mahakama iliamuru Kanisa kuondoa vigingi vya mipaka (beacons) walivyoweka na kuwalipa fidia ya Sh500 milioni kwa ajili ya kuwasumbua na kuwadhalilisha Sanga na wenzake.
Mgogoro huo ulianza baada ya mjibu maombi katika maombi hayo ambaye ni Baraza la Wadhamini kudai eneo lake hilo limevamiwa na wananchi hao na mwaka 2012 likawa linafanya kila aina ya jitihada ili kulichukua tena.
Inaelezwa katika mwenendo wa shauri hilo kuwa, Kanisa lilichukua uamuzi wa kijasiri wa kuweka alama za mipaka na katika kufanya hivyo, wananchi hao walitakiwa kuondoka katika eneo hilo, lakini wakakanusha kuwa wao ni wavamizi.
Asili ya mgogoro huo ilianza mwaka 2014 wakati Kanisa lilipomshitaki Agathon Duwe na wenzake 11 kupitia kesi ya ardhi namba 1 ya 2014 iliyofunguliwa Mahakama Kuu Songea, kanisa likidai ni mmiliki halali wa hekari 1,839.02.
Kesi hiyo ilimalizika nje ya mahakama na katika kesi mpya namba 5 ya 2021 iliyotolewa hukumu Machi 19 mwaka huu na Jaji Karayemaha, wananchi hao katika maombi yao walisisitiza kuwa ardhi hiyo hekari 1,160 haina uhusiano na kesi ya 2014.
Wakati wananchi hao wakieleza hivyo, Kanisa lilieleza ardhi iliyohusika katika kesi namba 1 ya 2014 inatambuliwa kwa hati ya umiliki namba 1431 land office namba 1182912, kiwanja namba 463 kilichopo kitalu “Liganga”.
Kupitia kiapo kinzani, Kanisa linadai ndio mmiliki halali wa eneo hilo na kuwataja waombaji (wananchi) kuwa ni wavamizi, lakini wananchi wao kitendo cha kanisa kutumia polisi kuwaghasi na kuwasumbua ndio kiliwafanya wakose uvumilivu.
Hukumu ya Jaji inasemaje
Hata hivyo, katika hukumu yake na baada ya kuchambua hoja za pande mbili, Jaji amesema umiliki wa wananchi hao unategemea namna wanavyothibitisha , lakini wajibu ambao wameshindwa kufanya hivyo katika shauri hilo.
Jaji amesema pamoja na wananchi hao kueleza waligawiwa eneo hilo na Serikali ya kijiji lakini hakuna ushahidi madhubuti kuthibitisha hilo, huku akisema mmoja wa mashahidi alielezwa na mtu mwingine kuwa walipewa ardhi na kijiji.
Kama hivyo ndivyo, Jaji amesema ni hatari sana kuamini ushahidi wa aina hiyo ambao hauwezi kuaminiwa na akasema hata hoja kuwa walirithi maeneo kutoka kwa wazazi wao, wote walitakiwa watoe ushahidi wao badala ya kumtegemea Sanga.
Jaji amesema,”nafikiri ilikuwa salama ushahidi wao wote (waleta maombi) kuwa katika kumbukumbu za Mahakama. Hii ingesaidia kuongezea nguvu madai yao na kutoa mwanga wa ni kwa nani walirithi na ukubwa wa eneo ungewekwa wazi.”
Kuhusu hoja ya baadhi ya waombaji kuwa waliyanunua, Jaji amesema hakuna ushahidi kuthibitisha hilo na pia hakuna aliyeita shahidi kuthibitisha ndiye aliyeuza, wala hapakuwa na mkataba wa mauziano uliotolewa mahakamani kama kielelezo kuthibitisha madai yao.
“Baada ya kueleza kuwa waombaji katika kesi hii sio wamiliki halali wa ardhi hiyo, kwa hiyo wajibu maombi (kanisa) wasingekuwa tena wavamizi wa ardhi yao wenyewe. Ninaona waombaji wameshindwa kuthibitisha madai yao,”amesema Jaji.
“Mahakama inatamka kuwa waombaji ni wavamizi wa eneo hili kwa hiyo wanaamriwa kuondoka. Fidia ya Sh420 milioni iliyoombwa na wajibu maombi hawajaweza kuithibitisha hivyo mahakama haiwezi kuwapa,”ameeleza.