Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kanda maalum kushughulikia migogoro ya ardhi Morogoro yaanzishwa

Kanda maalum kushughulikia migogoro ya ardhi Morogoro yaanzishwa

Fri, 6 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Waziri wa Ardhi nchini Tanzania, William Lukuvi amesema kutokana na kukithiri kwa migogoro ya ardhi Mkoa wa Morogoro Serikali imeunda kanda maalumu ya ardhi kwa ajili ya kuitatua.

Ametoa kauli hiyo jana Jumatano Desemba 5, 2019 wakati akijibu hoja mbalimbali wa wadau kwenye  mkutano kati ya mawaziri na wafanyabiashara mkoani Morogoro.

Lukuvi amesema lengo la kanda hiyo ni kumaliza changamoto zote za ardhi kati ya wafugaji na wakulima pamoja na mipaka.

Amesema Mkoa huo umekithiri migogoro ya ardhi na kuathiri shughuli za uzalishaji na uchumi.

Amesema kabla ya kuanzishwa kwa kanda hiyo, zilifunguliwa ofisi za ardhi kwa ajili ya Mkoa huo na Pwani kwa ajili ya kusikiliza mashauri madogo ya migogoro hiyo.

“Kutokana na uzito wa Mkoa wa Morogoro Rais John Magufuli alielekeza  kuundwa kwa kanda maalumu  kwa ajili ya mkoa huu ambayo kila kitu kitafanyika hapahapa  bila kufika makao makuu ya Wizara  na watumishi wa idara zote watapatikana hapa,” amesema Lukuvi.

Amesema pamoja na maelekezo hayo, Serikali imeshapitia mradi wa matumizi bora ya ardhi, kupima kila kipande cha ardhi katika wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi.

Amesema katika maeneo hayo hati 300,000 za kimila zimeshatolewa.

“Watu wa Morogoro wamependelewa katika mpango wa matumizi bora ya ardhi kuliko Mikoa mingine na wizara nayo kwa kupitia bajeti yake imetekeleza mpango wa upimaji wa matumizi ya ardhi katika vijiji mbalimbali vilivyokithiri migogoro ya ardhi halmashauri ya Wilaya ya Mvomero,” amesema Lukuvi.

Chanzo: mwananchi.co.tz