Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampuni ya Utalii yatoa gari la doria

36549 Pic+doria Kampuni ya Utalii yatoa gari la doria

Mon, 14 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori (WMA) ya Makao iliyopo wilaya ya Meatu, imepatiwa msaada wa gari aina ya Toyota Land Cruiser baada ya kusaini mkataba wa miaka mitano wa utalii picha na uwindaji na kampuni ya Mwiba Holdings Limited.

Kutokana na mkataba huo wa tatu kusainiwa baina ya hifadhi hiyo na Mwiba, Makao WMA itakuwa ikipata fedha wastani wa shilingi 600 milioni kutoka Sh400 milioni za miaka mitano iliyopita.

Akizungumza katika makabidhiano ya gari hilo, lenye thamani ya Sh40 milioni, baada ya kusaini mkataba, meneja wa Mwiba Holdings, moja ya kampuni ya Friedkin Conservation Fund, Mark Ghaui amesema wanatarajia ndani ya miaka mitano kuongeza watalii katika eneo hilo.

“Tumetoa msaada huu wa gari ili litumike katika doria za ulinzi wa wanyamapori na mazingira na tutaendelea kutoa misaada mingine ili kuhakikisha jamii pia inanufaika na uhifadhi,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu wa Makao WMA, Robert Simon alisema licha ya kushukuru kwa msaada huo, pia alitangaza operesheni ya kuwaondoa watu waliovamia maeneo ya hifadhi.

Simon amesema wametoa mwezi mmoja kwa kaya zaidi ya 60 zilizovamia maeneo ya hifadhi ili kutoka na hivyo kuendelea kutunzwa kwa mazingira ya hifadhi hiyo.

Amesema mkataba waliosaini, umeboreshwa kwani fedha za kila kijiji zimeongezeka kutoka wastani wa Sh25 milioni hadi 27 milioni na kwa mwaka fedha zimeongezeka hadi kufikia Sh600 milioni. Kaimu Mwenyekiti wa Makao WMA, Nzemo Gwesere aliipongeza kampuni ya Mwiba kwa kusaini mkataba mpya na Makao WMA na kutoa gari kwa ajili ya ulinzi.



Chanzo: mwananchi.co.tz