Dar es Salaam. Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, imepewa msaada wa Sh50 milioni na Kampuni ya National Aviation Service (Nas) Dar Airco ili kusaidia ujenzi wa nyumba za watumishi wa sekta ya afya.
Hundi ya fedha hizo imekabidhiwa leo Ijumaa Julai 12, 2019 na Meneja Mkuu wa kampuni hiyo inayojishughulisha na upakiaji na ushushaji mizigo kwenye viwanja vya ndege, Miguel Serra kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilolo, Aloyce Kwezi na Mkuu wa wilaya hiyo, Asia Abdallah.
Akizungumza kabla ya kukabidhiwa hundi hiyo, Kwezi amesema fedha hizo zitakwenda kuongeza nguvu ili kufanikisha ujenzi wa nyumba za watumishi watakaohudumia Hospitali mpya ya wilaya inayotarajiwa kuzinduliwa Septemba mwaka 2019 na Rais wa Tanzania, John Magufuli.
Amesema hospitali hiyo iliyoanza kujengwa mwaka 2016 ni ya kisasa na imekuwa ya mfano ambapo viongozi mbalimbali wamekuwa wakifika kujifunza jinsi ilivyojengwa.
“Malengo yetu ilikuwa tuwe na hospitali ya kisasa, tumekuwa tukitumia mikakati mbalimbali ikiwamo kushirikisha wadau wa maendeleo ikiwamo Nas ambao wamejitolea na hili tunashukuru sana sana,” amesema Kwezi
Naye Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Miguel Serra amesema licha ya kujikita kutoa huduma kwenye viwanja vya ndege lakini wanajielekeza maeneo mengine ya kijamii kama sekta ya afya, elimu na utalii.
Pia Soma
- Trump athibitisha wahamiaji kusakwa, kurejeshwa kwao wikiendi hii
- KESI YA KINA KITILYA: Watuhumiwa wawili kesi ya Kitilya wakataa tuhuma zote
- Mashabiki, wapinzani wa rais wa Taiwan watwangana nje ya hoteli aliyofikia Marekani
Serra amesema kwenye eneo la utalii, wanakusudia kuvitangaza vivutia vya utalii vya Tanzania katika maeneo mbalimbali duniani ambako wanatoa huduma ili kuwavutia watalii wengi zaidi kuja kuvitembelea.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Asia Abdallah licha ya kupongeza kwa msaada huo lakini ameikaribisha kampuni hiyo kwenda kuwekeza mkoani Iringa ambako kuna vivutio mbalimbali vya utalii.
Naye Mjumbe wa Bodi ya Nas Afrika, Balozi Costa Mahalu amesema kampuni hiyo imekuwa ya mfano kwani licha ya kutoa misaada kwa jamii, lakini imeajili asilimia 99 ya wafanyakazi wake ni wazawa.
“Hii kampuni ni ya mfano, ajira zake asilimia 99 ni wazawa, wameweka kipaumbele kwa wazawa na kusaidia jamii kwenye huduma za afya, elimu na utalii ambapo wataanza kuutangaza utalii wa Tanzania maeneo mbalimbali duniani,” amesema Balozi Mahalu ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustine (Saut)