Lindi. Serikali ya Tanzania imeridhia kampuni ya uchimbaji madini ya Graphite ya Lindi Jumbo kuanza ujenzi wa mitambo kwa ajili ya kuanza uzalishaji.
Hayo yameelezwa jana Jumatano Agosti 20, 2019 na naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo mjini Dodoma baada ya kukutana na mkurugenzi wa kampuni hiyo, Allan Mulligan.
Mulligan alimtembelea naibu waziri huyo kwa lengo la kumtaarifu kuhusu hatua iliyofikiwa katika mchakato wa ujenzi wa mitambo, mabwawa ya maji taka na miundombinu.
Amesema Serikali inahitaji fedha kwa ajili ya wananchi wake ndio maana inahimiza uzalishaji huo uanze ili kupata mapato.
Nyongo amemshukuru mkurugenzi huyo kwa kukamilisha ulipaji wa fidia kwenye maeneo yote ya mgodi, taratibu zinazohitajika kufuatwa kabla ya kuanza uzalishaji ikiwemo ujenzi wa bwawa la maji sumu (TFS).
“Hatupendi kuona migogoro kati ya mwekezaji na wananchi hasa katika masuala ya fidia kama ilivyotokea kwenye baadhi ya migodi, hongereni sana. Sasa nendeni mkafanye hima kukamilisha miundo mbinu na ujenzi wa plant ili muanze uzalishaji,” amesema Nyongo.
Pia Soma
- Majeruhi ajali gari la Tanapa wahamishiwa Bugando, Arusha
- Sheria mpya yazibana taasisi 258, zatakiwa kufanya usajili upya
- Benki ya Dunia kuikopesha Tanzania Sh3.9 trilioni
Mkurugenzi huyo amemjulisha Nyongo kwamba kwa sasa kampuni husika inafanya matengenezo ya barabara na miundombinu mingine na itakapofika Oktoba 2019, ianze ujenzi wa mitambo.