Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampeni kumtetea mwanamke amiliki ardhi kuzinduliwa

Kampeni kumtetea mwanamke amiliki ardhi kuzinduliwa

Thu, 14 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro . Licha ya Tanzania kuwa na sera na sheria zinazotoa fursa sawa ya kumiliki ardhi kwa jinsia zote lakini bado wanawake wanakutana na changamoto kumiliki rasilimali hiyo.

Kufuatia hilo taasisi na asasi zisizo zisizo za kiserikali 25 zimekuja na kampeni ya ‘Linda Ardhi ya Mwanamke’ inayolenga kutoa elimu kwa jamii kuhusu nafasi ya mwanamke katika kumiliki ardhi.

Kampeni hiyo ambayo pia itakwenda kwenye mataifa mbalimbali, itazinduliwa nchini Novemba 21, 2019 chini ya uratibu Shirika la Kimataifa la Landesa Tanzania.

Mwanasheria wa Landesa Tanzania, Godfrey Massay amesema kuna ombwe kubwa kati ya sheria na sera zinazohusu umiliki wa ardhi na utekelezaji wake kwa wanawake.

Alisema mila na desturi kandamizi nazo zimekuwa kikwazo kwa mwanamke kumiliki ardhi hivyo kampeni hiyo inakuja kubadili mtazamo hasi kuhusu umiliki wa rasilimali hiyo.

Alisema mwanamke anayemiliki ardhi ana uwezo wa kutumia ardhi hiyo kujikwamua kiuchumi na kuendesha familia.

"Watanzania wake kwa waume wana haki ya kumiliki ardhi ila tunataka wanawake wapewe fursa ya kumiliki ardhi hiyo ili iwaletee maendeleo chanya katika familia zao kwa kuwaongezea kipato na hili linawezekana."

Kwa upande wake mwanahabari mkongwe na mmoja wa wakurugenzi bodi ya Landesa, Edda Sanga alisema waandishi  wa  habari wana nafasi kubwa ya kutumia kalamu zao kuhakikisha kampeni hiyo inafanikiwa.

Alisema mipango na sera zilizopo zikitekelezwa inavyostahili migogoro ya ardhi na malalamiko ya wajane kunyang’anywa ardhi na mali yatapungua.

Alisema ipo haja  ya kuhakikisha sheria na sera zinatekelezeka kwa kuwa wanawake wengi ndio wanaoshiriki kikamilifu katika kilimo hivyo wasipopata nafasi ya kumiliki ardhi yale yanayosema kwamba wanayaweza hawataweza kuyafanya.

"Kampeni hii si rahisi kama tunavyofikiria bali ni ngumu kwani bado jamii nyingi hazioni umuhimu wa mwanamke kumiliki ardhi, hivyo waandishi tumieni ubunifu kuondokana na dhana potovu waliyonayo kwa wanawake," alisema.

Kampeni ya Linda Ardhi ya Mwanamke itazinduliwa Novemba 21 jijini Dar es Salaam, mgeni rasmi katika uzinduzi huo atakuwa Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Chanzo: mwananchi.co.tz