Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampeni dhidi ya mimba, ndoa za utotoni yaanza Mkuranga

33084 MIMBA+PIC Tanzania Web Photo

Sun, 23 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mkuranga. Shirika lisilo la Kiserikali linalojihusisha na masuala ya kisaikolojia nchini (REPPS) limeanza kampeni ya kupambana na tatizo la mimba na ndoa za utotoni baada ya tafiti nyingi kuonyesha bado tatizo hilo ni kubwa.

Takwimu za Democratic and Health Survey, zinaonyesha tatizo la mimba za utotoni nchini limeongezeka kutoka asilimia 23 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 27 mwaka 2016/17, kutokana na ukosefu wa huduma pamoja na elimu ya afya ya uzazi kwa vijana wa umri kuanzia miaka 15 hadi 19.

Mkurugenzi Mkazi wa Repps Tanzania, Edwick Mapalala amesema kampeni hiyo wanaiendesha kwa kuzungumza na jamii kwenye vijiwe, shambani, maeneo ya masomo na mikusanyiko yote ili kufikisha elimu ya namna ya kuwalea na kuwatunza watoto kimaadili.

“Tatizo la mimba na ndoa za utotoni lipo kwenye jamii yenyewe, wazazi na walezi wakijua umuhimu wa malezi bora tatizo hili halitakuwepo kabisa,” amesema.

Amesema kama watoto wa kike wataendelea kukatisha masomo yao kwa mimba na ndoa itakuwa vigumu kufikia ndoto ya Tanzania yenye viwanda kwa sababu nguvu kazi inayoachwa njiani ni kubwa.

“Mtoto wa kike akipata elimu na kusoma kwa bidii atatimiza ndoto yake na kuja kuchangia maendeleo kwenye taifa lake,” amesisitiza.

Amesema kupitia kampeni hiyo wanayoiendesha kwa ushirikiano na shirika lililo chini ya Kanisa Katoliki jimbo kuu la Dar es Salaam (Pasada), vijana wameweza kupewa elimu ya afya ya uzazi na kujitambua itakayowasaidia kufikia ndoto zao.

Kaimu ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Parang’anda, Felisian Magulu amesema kupitia kampeni hizo jamii inapata ufahamu wa madhara ya mimba kwa watoto na kujua namna ya kupambana na tatizo hilo.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkuranga, Dunia Mabufu alikiri kuwepo kwa kampeni za aina hiyo kunasaidia katika kubadili fikra za wengi zinazoendeshwa na mila na desturi kandamizi dhidi ya wasichana na wanawake.



Chanzo: mwananchi.co.tz