Wananchi wa Mkoa wa Lindi wameishukuru Serikali baada ya kutangaza rasmi kuanza kwa ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mapema mwezi Desemba mwaka huu katika eneo la Gongo kata ya Jamhuri mkoani humo.
Wananchi hao wasema hayo walipokutana na kuzungumza na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia juu ya utekelezaji wa mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unaofadhili ujenzi wa Kampasi hiyo.
Pia wameiomba Serikali kuhakikisha wakandarasi watakaotumika kujenga chuo hicho kuhakikisha wanatekeleza kazi hiyo kwa weledi na kukamilisha kwa wakati ili Chuo kiweze kuanza kama ilivyopangwa huku wakishukuru kushirikishwa toka hatua za awali za mradi.
Akitangaza kuanza kwa ujenzi huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kujengwa kwa kampasi hiyo ni maelekezo ya Mhe. Rais kuhakikisha mikoa yote ambayo haina vyuo vikuu inajengewa kampasi za vyuo vikuu.
Ametaja mikoa mingine itakayojengewa kamapsi za Vyuo Vikuu kuwa ni Kagera, Mwanza, Shinyanga, Singida, Manyara, Tanga, Simiyu, Kigoma, Ruvuma, Rukwa Katavi, na Zanzibar (Institute of Marine Scince) na kwamba kampasi hizo zinajengwa na Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).
Waziri Mkenda amevitaka Vyuo vikuu vitakavyojenga kampasi hizo kuzielekeza kwenye kutoa mafunzo ya amali lakini pia kufanya tafiti. Aidha amekipongeza Chuo Kikuu kwa kukamilisha taratibu hizo lakini pia Mkoa wa Lindi kwa kutoa ushirikiano wa kuhakikisha ujenzi wa chuo hicho unaanza.
Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mkuu wa wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga ameishukuru Serikali na ameeleza kuwa tayari Mkoa umewezesha upatikanaji wa eneo zaidi ya ekari 492 na ameahidi kwa niaba ya Mkoa kutoa ushirikiano kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kama ilivyopangwa.