Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi katika Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Humphrey Habakuki na askari ambaye ni dereva wa shirika hilo, Isack Nassari wamefariki dunia papo hapo baada ya gari walilokuwa wanasafiria kugongana uso kwa uso na gari la Tanesco katika eneo la Bwawani mkoani Morogoro.
Habakuki na mwenzake walikuwa wanasafiria kutoka Dar es Salaam kwenda Mikumi.
Akizungumza kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema ajali hiyo imetokea jana na kwamba chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa gari la Tanapa kutaka kulipita gari jingine bila ya kuchukua tahadhari.
"Huyu dereva wa Tanapa ambaye kwa sasa ni marehemu alitaka kulipita gari jingine, tena katika eneo lenye kona kali bila ya kuchukua tahadhari, ndipo alipokutana na lori la Tanesco na kugongana uso kwa uso," amesema Kamanda Mkama.
Ametaja waliojeruhiwa katika ajali hiyo kuwa ni David Mwapongo (38) ambaye ni dereva wa Tanesco jijini Dar es Salaam na Sostenes Buyekwa (40) ambaye ni mfanyakazi wa Tanapa Mikumi ambao wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro. Miili ya marehemu pia imehifadhiwa katika hospitali hiyo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kusirye Ukio amethibitisha kupokea miili hiyo pamoja na majeruhi ambao wanaendelea na matibabu.
"”Usiku wa kuamkia jana ( Machi 24) tumepokea miili miwili ya marehemu wa ajali hiyo pamoja na majeruhi wawili ambao bado tuko nao na tunawapatiwa matibabu na uangalizi wa karibu," amesema Ukio.
Taarifa iliyotolewa jana Jumapili Machi 24 na Kamishna wa Uhifadhi Tanapa, Mussa Kuji imesema: “Kwa niaba ya Tanapa natoa pole kwa familia, maofisa na askari wa Jeshi la Uhifadhi, ndugu, jamaa na marafiki wote. Mwenyezi Mungu azilaze pema peponi na majeruhi apone haraka.”