Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kamati yaundwa kuleta suluhu mgogoro wa ardhi Chamwino

Aed14a968476d9ab3a8722cfa6e188ca Kamati yaundwa kuleta suluhu mgogoro wa ardhi Chamwino

Fri, 5 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge ameuvalia njuga mgogoro wa ardhi kati ya Halmashauri ya Chamwino na wanakijiji wa Mwegamile, Kata ya Buigiri wilayani Chamwino kwa kuunda kamati maalumu kuyachunguza malalamiko .

Wanakijiji wanadai mwekezaji aliyepewa ekari 400 kujenga kiwanda cha kukamua zabibu amemega eneo lao. Dk Mahenge ameamua kuumaliza mgogoro huo ambao umekuwa ukijirudia na kuleta kutolewana kutokaa na dai kuwa Halmashauri ya Chamwino imekuwa ikitoa eneo la Chinangali II kwa wawekezaji bila kijiji kushirikishwa na wananchi kulipwa fidia.

Akizungumza baada ya kumsikiliza mwakilishi wa wanakijiji, wakili Gabriel Masinga na Mkuu Idara ya Kilimo Halmashauri ya Chamwino, Godfrey Mnyamale, Dk Mahenge alisema anaunda kamati maalumu.

Kamati hiyo itaongozwa na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Maduka Kessy na kushirikisha Takukuru, halmashauri, wizara ya ardhi, wawakilishi wa wananchi na itafanya kazi kwa siku 14.

Dk Mahenge akizungumza mbele ya Mbunge wa Jimbo la Chamwino ambaye pia ni Naibu Waziri,Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi aliipa kamati hiyo hadidu za rejea kwamba inatakiwa kuchunguza ili kuthibitisha uhalali vikao vya uamuzi na mihutasari ya vikao vya madiwani kuhusu kuridhia mwekezaji Mburugaria na Mtanzania baadaye Mmarekani kupewa maeneo na kushindwa kuyaendeleza na uhalali wa mipaka iliyopo na ukubwa wa eneo hilo.

Pia ilitakiwa kamati hiyo kujiridhisha kuhusu ekari 400 ambazo amepewa mwekezaji Kampuni ya Mega Beverage kwa ajili ya kuanzisha kiwanda cha kuchakata zabibu na kama hazitaathiri shughuli za wakulima wadogo kutokana na ukweli kwamba eneo hilo ni mali ya serikali tangu Baraza la Madiwani wa CCM mwaka 1984 waliporidhia kuwa ni mali ya halmashauri hiyo.

“Japokuwa Halmashauri ya Chamwino haikutunza eneo hilo la hekta 500 sawa na ekari 1,622, tangu wamepewa na kikao halali cha Baraza la Madiwani mwaka 1984 ambapo waliridhia kumpa mwekezaji, ambaye aliahidi kutoa mchango wa maendeleo katika kijiji hicho kwa kujenga darasa kutokana na kutoa ardhi hata kama hakutekeleza wakati akisuburi uamuzi darasa lijengwe Chinangali II au Mwendamile,” alisema.

Awali, Kiongozi wa Wananchi walalamikaji wa Kijiji cha Mwendamile, Gabriel Masinga alisema wananchi wa kijiji hicho hawatakubali kutoa ardhi yao kwa mwekezaji huyo Mega Bavarage Limited K-Vant kutokana na kwamba hawakushirikishwa katika upangaji wa eneo hilo, kila wakati halmashauri hiyo imekuwa ikiongeza mipaka bila kuwashirikisha na kuwalipa fidia.

Alisema mgogoro huo ulianza mwaka 2007/08 kwa kutoa ekari 350 ili kuanzisha Mradi wa Kilimo Kwanza, lakini wananchi wake hawakupewa fidia na mbaya zaidi halmashauri hiyo ilipitisha michoro mipya Oktoba 7, 2011, bila kuwashirikisha wananchi.

Masinga alisema pia halmashauri hiyo katika kipindi cha mwaka jana walipitisha mchoro mwingine bila kuwashirikisha na kumpa mwekezaji Mega Bevarage ekari 400 ambaye hajafika ofisi ya kijiji, lakini ameanza kufyeka barabara katika mashamba yao na makaburi yao na katika maeneo yao ya kufugia.

Chanzo: www.habarileo.co.tz