Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kamati ya RC yapendekeza DC, DED wahamishwe

37647 KamatipicKamati ya RC yapendekeza DC, DED wahamishwe

Tue, 22 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Kamati iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira kuchunguza mgogoro wa kiuongozi wilayani Mwanga imependekeza mkuu wa wilaya hiyo (DC), Aaron Mbogho na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya (DED), Zefrin Lubuva waondolewe ama wote au mmoja wao.

Mghwira aliamua kuunda kamati hiyo kwenda kuchunguza mgogoro huo baada ya hivi karibuni Lubuva kudaiwa kupigana ofisini na ofisa mmoja wa wilaya hiyo, jambo lililozua sintofahamu ya kiuongozi wilayani humo.

Hatua ya viongozi hao wa Serikali kupigana ofisini ilielezwa kuwa ni baada ya mkurugenzi kutohudhuria kikao kimoja kilichokuwa kimepangwa kufanyika Januari 17, huku akituma mwakilishi.

Akizungumzia na Mwananchi kuhusu mapendekezo ya kamati aliyounda, Mghwira alisema wakurugenzi, wakuu wa wilaya pamoja na watendaji wengine wa Serikali mkoani humo wanapaswa kufanya kazi kwa kushirikiana na si kuendeleza migogoro ambayo haina tija.

“Kamati iliyokwenda kufanya uchunguzi imeshakuja na (ripoti) tunaifanyia kazi,” alisema mkuu huyo wa mkoa.

“Kwa hiyo tumebakiwa na mapendekezo mawili; waondolewe wote wawili kama hawawezi kufanya kazi kwa pamoja au mmoja wao aondolewe, tuone kama wakitofautishwa kazi inakuwa nafuu.”

Alisema mgogoro uliopo wilayani Mwanga na kitendo cha watendaji kupigana ofisini ni kufikia ukomo wa kufikiri na hakipaswi kufanywa na viongozi wa Serikali.

Alisema mawasiliano mazuri, uvumilivu na kuheshimiana kimamlaka ni jambo muhimu la kuzingatia kwani kutofanya hivyo kunachelewesha maendeleo ya wananchi.

Mkuu huyo wa mkoa alisema vikao vyote viwili ambavyo vilikuwa vifanyike Januari 17 vya kamati ya ulinzi na usalama pamoja na kile cha kamati ya Ukimwi wilayani humo vilikuwa ni muhimu na vilipaswa mkuu wa wilaya awepo pamoja na mkurugenzi. “Vikao vyote viwili vilipaswa mkurugenzi na mkuu wa wilaya wawepo, wangeweza tu kujipanga kwamba wafanye kikao kimoja kwanza wamalize kisha waingie kikao cha pili,” alisema Mghwira.

Mwananchi lilizungumza na Lubuva kuhusu mapendekezo hayo lakini alisema hawezi kusema lolote kwa kuwa jambo hilo liko katika mamlaka za juu.

Alipoulizwa sababu za kutohudhuria kikao cha kamati ya ulinzi na usalama cha wilaya, alisema kulikuwa na kikao kingine cha kamati ya Ukimwi ambacho alipaswa kukifanya kama mkurugenzi na kilikuwa kinajulikana.

“Mimi nilikuwa kwenye kikao cha kamati ya Ukimwi, muda mfupi nikiwa kwenye kikao nililetewa kinoti kilichoandikwa kwa mkono, kwamba napaswa kuhudhuria kikao cha ulinzi na usalama,” alisema Lubuva.

“Ilinibidi nimtume mwakilishi wangu kwa barua nikijua siyo haramu kufanya vile, lakini kilichotokea walitaka kunitoa kwenye kikao kwa nguvu, tena walitaka kunibeba juu juu.”

Alisema baada ya kutokea vurugu katika kikao kile alipigwa na baada ya ugomvi wao kuamuliwa na watumishi wa halmashauri hiyo alikwenda polisi kutoa taarifa.

“Mimi nilipigwa siyo kwamba tulipigana na ndiyo maana baada ya kuamuliwa na watumishi wa hapa (wilayani) nilikwenda polisi kutoa taarifa,” alisema.

Jitihada za kumpata DC Mbogho kuzungumzia mapendekezo ya kamati ya mkuu wa mkoa jana, hazikufanikiwa.

Hivi karibuni, mkuu huyo wa wilaya aliagiza polisi kumkamata Lubuva na kumuweka mahabusu kwa madai ya kutotekeleza maagizo yake.

Pia, aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kumchunguza mtendaji huyo pamoja na kaimu mtendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mwanga, Justine Valentino.



Chanzo: mwananchi.co.tz