Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kamati ya Bunge yampa agizo mkandarasi ujenzi daraja la mto Kagera

Mkandarasi Bunge Kamati ya Bunge yampa agizo mkandarasi ujenzi daraja la mto Kagera

Mon, 21 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Moshi Kakoso amemtaka mkandarasi anayejenga daraja la Kitengule lililopo mto Kagera kukamilisha ujenzi kwa wakati ili kufungua fursa za kiuchumi kwa wakazi wa wilaya za Karagwe na Misenyi mkoani Kagera.

Ameyasema hayo jana Machi 20, 2022 wakati kamati hiyo ikiwa imeambatana na Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya kutembelelea daraja hilo kuona maendeleo ya ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 140.

"Kamati tunaomba mkandarasi wa daraja hili China Henan International Cooperation Group Co Ltd (CHICO) kumaliza mradi huu ifikapo Mei 26 mwaka huu" amesema Kakoso

Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Kagera, Mhandisi Yudas Msangi amesema daraja hilo limeanza kujengwa Oktoba 2018 na ujenzi unatarajia kukamilika Mei 2022 na kuwa ujenzi wa daraja umekamilika kwa 97 asilimia na ujenzi wa barabara unganishi kilomita 18 unaendelea umefikia 36.8 asilimia.

Mhandisi Msangi amesema mradi uko nyuma kwa asilimia 2.92 kutokana na changamoto zilizojitokeza wakati wa kuutekeleza ikiwa ni pamoja na kucheleweshwa kutolewa hati ya msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT), mlipuko wa ugonjwa wa uvico-19 na mvua zilizonyesha juu ya wastani.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya ameeleza kwamba mwezi Februari mwaka huu Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa alipita katika barabara unganishi na daraja la Kitengule na kuagiza barabara hizo zinazounganisha daraja zenye urefu wa kilomita 18 zijengwe kwa kiwango cha rami na kwa sasa usanifu umefikia 80 asilimia.

Mhandisi Kasekenya amezitaja barabara nyingine ambazo zitajengwa Kagera kwa kiwango cha rami kuwa ni barabara ya Bugene Ngara na barabara ya Omurushaka Kaisho ambazo tayari zimeishatangazwa ikiwemo ya Omugakorongo Murongo ambazo kukamilika kwake kutafungua fursa za kiuchumi mkoani Kagera

Chanzo: www.tanzaniaweb.live