Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kama una nyumba haina choo mkoani Kagera kazi unayo

59505 Choopic

Fri, 24 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bukoba. Mkuu wa Mkoa wa Kagera,  Brigedia Jenerali Marco Gaguti ametangaza msako mkali kwa kaya zisizo na vyoo baada ya Agosti 30, 2019.

Akizungumza na  waandishi wa habari leo Ijumaa Mei 24, 2019 kuhusu kampeni ya kitaifa ya "Usichukulie poa nyumba ni choo",  Gaguti amesema baada ya tarehe hiyo msako mkali utafuata.

Kampeni hiyo kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa itazinduliwa kesho Jumamosi Mei 25, 2019 katika uwanja wa Kaitaba na timu ya uhamasishaji na utoaji wa elimu itakayoongozwa na msanii, Mrisho Mpoto.

Pia, Brigedia Gaguti ameagiza halmashauri zote za Wilaya kuwasilisha matamko kwa maandishi wakionyesha jinsi watakavyotekeleza agizo hilo la msako kwa kaya zisizo na vyoo.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa Mkoa wa Kagera asilimia tano ya wakazi wa Mkoa huo hawana vyoo na kwamba agizo lake linalenga kutokomeza tatizo hilo katika baadhi ya kaya.

Mratibu wa kampeni ya Taifa ya usafi wa mazingira, Anyitike Mwakitalima kutoka  Wizara ya Afya amesema tangu kuanza kwa kampeni hiyo mwaka 2012 kasi ya   ugonjwa wa kuhara limepungua kutoka watu 1.4 milioni hadi 70,000 na kutaka wananchi kuitikia wito wa kuwa na vyoo pamoja na kuvitumia.

Pia Soma

Amesema lengo la kitaifa ni kuwa na kaya asilimia themanini zenye vyoo bora ifikapo 2020 na kuwa mapitio ya takwimu yaliyofanyika yanaonyesha mafanikio makubwa kupitia kampeni hiyo.

Hata hivyo,  changamoto ya ukosefu wa vyoo inaonekana kwenye kaya za visiwa vya ziwa Victoria na Gaguti amesema ni wajibu wa kila mtu kwa nafasi yake kuhakikisha kampeni hiyo inamfikia kila mwananchi.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz