Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kalemani aipa Tanesco miezi 6 Dodoma yote kupata umeme

9c7fa43ea7359f2d44e96183da79b97c Kalemani aipa Tanesco miezi 6 Dodoma yote kupata umeme

Mon, 25 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI wa Nishati, Dk Medard Kalemani, ameliagiza Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) mkoani Dodoma kuhakikisha ndani ya miezi sita kuanzia sasa, vijiji na maeneo yote ya mkoa huo yawe yameunganishwa na kupata nishati ya umeme na kwamba atakayeshindwa kutekeleza hilo, atakuwa amejifukuza kazi mwenyewe.

Alisema hayo katika mkutano na wafanyakazi wa Tanesco wa Mkoa wa Dodoma uliolenga kufahamiana, kusikiliza changamoto zinazowakabili wafanyakazi pamoja na kutoa maelekezo ya kuboresha utendaji kazi wa shirika hilo.

Alisema wafanyakazi ndio wenye dhamana na jukumu kubwa kuhakikisha Mkoa wa Dodoma unapata umeme wa kutosha na wa uhakika katika maeneo yote sambamba na kuunganisha na kuwawashia umeme wateja.

Alisema kwa sasa Dodoma una wakazi wengi huku wengine wakiendelea kuingia kwa kuwa ni makao makuu ya nchi, hivyo umeme mwingi unahitajika katika shughuli mbalimbali.

Kutokana na hali hiyo, kila mfanyakazi wa Tanesco anapaswa kuwa sehemu ya shirika na afanye kazi kwa kasi zaidi, ubunifu mkubwa na kwa usahihi zaidi ili kuboresha huduma za Tanesco na kukidhi mahitaji ya umma.

“Sitakubali kupata aibu ya baadhi ya maeneo na vijiji vya makao makao ya nchi kutokuwa na umeme, mkoa huu una zaidi ya megawati 400 za umeme, lakini matumizi ni megawati 45 tu kwa sasa, wakati kuna wateja wengi wanaohitaji umeme na maeneo mengine bado hayajafikiwa kabisa na huduma hiyo, Tanesco Dodoma fanyeni kazi!,”alisisitiza Dk Kalemani katika mkutano huo wa Januari 22, mwaka huu.

Kalemani aliipa Tanesco mkoani Dodoma siku 14 kumfikishia taarifa za namna walivyojipanga kusambaza umeme kwa wananchi, kuunganisha wateja wa zamani na kupata wapya, kuzalisha na kusafirisha umeme katika maeneo mbalimbali nchini.

Alipiga marufuku watumishi wenye kasumba ya kuchelewesha majalada ya kazi, kwa kusema kuwa vitendo hivyo vinachelewesha utendaji kazi na kutotimiza malengo kwa wakati.

Kwa mujibu wa waziri huyo, asilimia kubwa ya utendaji kazi katika ofisi hufanyika kwa mfumo wa maandishi kupitia majalada, hivyo, endapo mtumishi mmoja atachelewa au kukwamisha, kazi husika itachelewa na kutotekelezeka kwa muda uliopangwa.

Katika hatua nyingine, Dk Kalemani aliiagiza Tanesco, kuangalia upya utaratibu wa kuajiri au kuwapa kazi wafanyakazi wa muda maalum (STE) ambao muda mwingi wanakuwepo maeneo kazikufanya kazi za kuchimba mashimo, kusimika nguzo na kuvuta nyaya.

Aliagiza wafanyakazi wasio na mikataba wapewe mikataba, wenye sifa ya ajira waajiriwe na wale wasiokuwa na sifa lakini wamefanya kazi muda mrefu, wapewe mafunzo maalumu ili wapate ajira.

Pia alitaka shirika hilo kuboresha maslahi wa wafanyakazi hao na kuangalia namna bora ya kuwapa motisha sehemu za kazi waweze kufanya kazi zao kwa furaha, amani na utulivu na kuboresha utendaji kazi wao.

Sambasamba hilo, alitoa miezi miwili kwa wapimaji na watathmini pamoja na watoa namba za malipo kwa wateja ili kulipia gharama za kuunganishiwa umeme, kubadilika na kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na taaluma zao, na atakayeshindwa kufanya hivyo afukuzwe kazi.

Akizungumzia kitengo cha huduma kwa wateja, Dk Kalemani alitaka wahusika kutumia lugha rafiki na zinazofaa kwa wateja, kuweka watoa huduma vijana ili wafanye kazi haraka zaidi.

Chanzo: habarileo.co.tz