Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kalemani: Magufuli alituandaa kifikra

39c47b00d8248b15f8c193a1f5dd9392 Kalemani: Magufuli alituandaa kifikra

Thu, 25 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MBUNGE wa Jimbo la Chato, Dk Medard Kalemani amesema miongoni mwa mambo makubwa na mazuri ambayo Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli aliwafanyia Watanzania, ni kuwandaa kujitegemea hata kifikra.

Dk Kalemani ambaye pia ni Waziri wa Nishati alisema hayo jana alipozungumza na HabariLEO kuhusu matarajio ya wananchi jimboni Chato baada ya kufariki dunia kwa Magufuli.

Hayati Rais Magufuli alifariki dunia Machi 17, mwaka huu mkoani Dar es Salaam kutokana na matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo.

Jumamosi na Jumapili, mwili wa marehemu uliagwa katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam kisha ukapelekwa Dodoma kwa mazishi ya kitaifa yaliyohudhuriwa pia na viongozi na wawakilishi kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Machi 23 (juzi), uliagwa na wananchi wa Zanzibar wakiongozwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na jana uliagwa na wananchi wa Mwanza na hatimaye kulala Chato ambapo leo itakuwa zamu kwa wananchi wa Chato kuaga na kutoa heshima za mwisho kabla ya kuzikwa kesho, Machi 26, 2021.

Kalemani alisema katika mazungumzo hayo kuwa, mbali na kutumia kipindi chake cha uongozi kuwatumikia Watanzania akiwa kiongozi mkuu wa nchi, pia alifanya jambo jema kwa kuliandaa taifa kufikia azma ya kujitegemea kiuchumi na kifikra.

Kwa mujibu wa Kalemani, enzi za uongozi wa Magufuli, aliwaandaa Watanzania kiasi cha kutosha kwa msisitizo wa kuchapa kazi ili kuondokana na utegemezi wa misaada na kuamriwa mambo ya kufanya.

Alisema Hayati Magufuli aliwaandaa viongozi na wawakilishi wa wananchi kufanya kazi kwa bidii, hivyo ni wajibu kwa Watanzani wote sasa, kuendelea kushikamana hata baada ya kifo cha Magufuli ili kuliimarisha zaidi taifa.

"Serikali ipo, tuendelee kuiamini, wawakilishi wa wananchi wapo tuendelee kuwaamini, Watanzania tupo, tuendelee kujiamini, tutembee kifua mbele kama ambavyo Magufuli alitusisitiza na tumtangulize Mungu mbele kama ambavyo mara zote alikuwa akitusisitiza.

"Tanzania itabaki kuwa moja, Watanzania tutabaki wamoja, na viongozi tuliopo tuziishi na kuzienzi fikra na maoni ya kiongozi wetu na mimi niseme wazi kwamba, Rais Magufuli alituandaa Watanzania kwa miaka yote kwa maana hiyo, hata sisi wananchi wa Chato tumejiandaa kuiendeleza Chato yetu na taifa kwa jumla,” alisema.

Akaongeza: "Kila mmoja anafahamu, Magufuli alikuwa jemedari, shupavu katika maamuzi, mwenye busara, mwenye maono, ambaye amefanya makubwa, ni matumaini yangu Watanzania tutaendelea kuyaenzi daima."

Alisema jambo la msingi kwa wananchi wa Chato ni kuenzi maono yake, matendo yake na fikra zake, ili zidumu huku Watanzania wakiendelea kumuombea kwa kuwa ni mtu aliyempenda Mungu na aliyekuwa na hofu kwa Mungu.

Alisisitiza kuwa, akiwa mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Chato, ataendelea kuwaunganisha ili wabaki imara na wamoja, wenye amani na upendo kwa taifa lao.

Kalemani aliwahakikishia Watanzania wenye kiu ya kuwekeza Chato kuwa, fursa zitaendelea kuwepo hivyo wazidi kujitokeza.

Chanzo: www.habarileo.co.tz