Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kaka wa 'house girl' anayedaiwa kunyongwa afunguka mazito

Screenshot 20230218 072223 Facebook Kaka wa 'house girl' anayedaiwa kunyongwa afunguka mazito

Fri, 17 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Imani Benjamin ambaye ni kaka wa msichana wa kazi za ndani, marehemu Anneth Kassim (20) anayedaiwa kuuawa nyumbani kwa bosi wake Tabata Kimanga jijini hapa, amejitokeza kuutambua mwili wa dada yake katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili leo Februari 17.

Baada ya kuutambua mwili huo, Benjamin amewasimulia waandishi wa habari namna alivyonusurika kuuwawa kabla hajafukuzwa na kumuacha mdogo wake kwa bodi huyo.

Benjamin ndiye aliyemleta mdogo wake kufanyakazi kwa Diana Joseph anayetuhumiwa kumuua Anneth Februari 8, 2023 majira ya saa mbili usiku nyumbani kwake na kumfikisha katika hospitali hiyo, akidai alimkuta binti huyo amejinyonga bafuni.

Taarifa ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Debora Magiligimba ilieleza kuwa Februari 9 majira ya saa 9:45 asubuhi ilieleza kuwa walipokea simu kutoka kitengo cha dharura Muhimbili wakielezwa utata wa kifo cha Anneth.

Benjamin amejitokeza leo asubuhi katika hospitali ya Muhimbili akitokea kijiji cha Mkikomelo kata ya Mgoma, wilaya ya Ngara kwa ajili ya kuutambua mwili wa ndugu yake kabla ya kuingia eneo la mochwari saa 4 asubuhi.

Baada ya kuingia ndani alionyeshwa mwili na kuutambua kabla ya jopo la madaktari kuanza kuufanyia uchunguzi (postmortem) ili kubaini chanzo halisi cha kifo kwa takribani saa kadhaa, ambapo Imani na binti wa Diana, Pendo Joseph walihojiwa na polisi.

Hata hivyo Imani amesema ilichukua kipindi cha wiki nzima kutafuta nauli ili aje kushuhudia mwili wa ndugu yake.

“Sikuwa na nauli taarifa nilipewa na Pendo (binti wa Diana) Ijumaa, nilimuuliza ameumwa akanijibu hapana ila mama ndiyo anadaiwa kumuua na yupo polisi kwa sasa.

“Tangu hapo nilikuwa nahangaika kutafuta nauli nifike Dar ili kuukagua mwili wa mdogo wangu. Nasikitika kwa kuwa mara ya mwisho nilizungumza naye Novemba mwaka jana tangu hapo sikumpata tena hewani.”

Katika Mahojiano ya kina na Mwananchi, Imani amebainisha kuwa kabla Aneth hajafika hapa jijini kufanya kazi za ndani yeye ndiye aliyekuwa akifanya kazi kwa Diana kama muuzaji wa viungo mbalimbali akitembeza mtaani tangu Mei mwaka 2022.

Imani alisema alikaa miezi mitatu na mwajiri wake na kwa kuwa kazi zilikuwa nyingi, Diana alimshawishi amlete mdogo wake kwa ajili ya kufanya kazi za ndani kwa mshahara wa Sh50,000 kama anaolipwa yeye na alikubali.

“Alikuja mwezi wa nane mwaka jana aliniacha nikaishi naye vizuri wiki moja baada ya hapo akaanza kuninyanyasa, nilikuwa nasingizwa mwizi nimeiba hela mara panya rodi siku hiyo niliibiwa boksi la nyanya alinirukia na kunikaba shingoni pumzi zilikuwa zinakata ikabidi niwe mpole akaniachia,” amesimulia.

Imani amesema kwa kuwa bosi wake alishamtenga na mdogo wake, hakuna na mtu wa kumsikiliza siku iliyofuata alimfukuza kwa kumpiga bila kumpa mshahara na akimdai fidia ya Sh40,000 ya fedha za nyanya zilizoibiwa.

Amesema kutokana na vitisho alivyokuwa akipewa alishindwa kufika polisi wala kushtaki kwa Mjumbe ilimlazimu aondoke kurudi Ngara na baadaye alitafuta hizo fedha na kumlipa Diana kama fidia.

Tangu hapo amesema hakuwahi tena kuongea na mdogo wake, “Mara ya mwisho kuongea na mdogo wangu ilikuwa Novemba mwaka jana hakuniambia chochote baada ya hapo hatukuwasiliana tena.

“Leo nimemuona akiwa maiti na alama shingoni kama mtu aliyejinyonga kwa kutumia kamba kinachoniuma anasema wiki moja kabla aliwasiliana na baba jambo ambalo si kweli tulikuwa tukimpigia anakata simu na wakati mwingine anatukana na simu ya mdogo wangu ilikuwa haipatikani,” amesema Imani.

Hata hivyo, Diana anayetuhumiwa kumuua Aneth, ameelezwa kuwa alikuwa akifanya vitendo vya unyanyasaji wa kipigo kwa wajukuu zake na wafanyakazi kwa kipindi kirefu.

Tukio hilo ni mwendelezo wa matukio kadhaa ya kikatili ambayo yamekuwa yakifanywa na Diana na kushuhudiwa na majirani kwa vipindi tofauti tangu mumewe Joseph Mwita alivyofariki mwaka 2017.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live