Mabasi mawili ya abiria yamegongana eneo la Phantom, Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, huku abiria waliokuwa wakisafiri kutoka Arusha Kwenda Kahama na Karagwe mkoani Kagera wakinusurika kifo.
Ajali hiyo imetokea leo Jumapili, Machi 3, 2024 saa 11 jioni baada ya basi la kampuni ya Marangu Coach kugongana na basi la kampuni ya Mumuk Investiment katika eneo hilo.
Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Francis Maige amedai, “Hawa madereva wote wanamakosa maana haiwezekani umeshafika mjini unaelekea stendi ushindwe kuchukua tahadhari, matokeo yake unakuwa na haraka na kusababisha ajali.”.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema ajali hiyo imesababishwa na uzembe wa madereva wote wawili, hakuna kifo kilichotokea.
Kamanda Magomi amesema madereva hao watawafungia leseni zao ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.