Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kagera yaongoza kwa matukio ya mauaji, kujinyonga

Kaimu Kamanda Wa Polisi Mkoa Wa Kagera ACP Maketi Msangi Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kagera, Maketi Msangi

Tue, 28 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kagera, Maketi Msangi amesema mkoa huo unaendelea kuongoza kwa matukio ya mauaji, kujinyonga na kujeruhi, ambapo kwa kipindi cha mwaka jana kulikuwa na matukio yasiyopungua 190

Akizungumza katika kikao cha kujadili namna gani ya kukabiliana na vitendo vya mauaji, kilichoitishwa na Kamishna wa polisi jamii Tanzania na kuwashirikisha viongozi wa dini, kimila, wazee maarufu askari na watendaji wa kata kamanda Msangi amesema Mkoa unaongoza katika matukio makubwa ambayo yanavuta hisia za wananchi na wakati mwingine kupunguza hamasa kwao, ya kwenda kujitafutia riziki.

“Lakini kuna Wilaya ambazo zinaongoza kwa mfano Wilaya ya Muleba kwa mwaka jana pekee kulikuwa na matukio 40, ikifuatiwa na Ngara matukio 36 na ya tatu ni Bukoba matukio 30” amesema Msangi

“Kumejitokeza matukio hivi karibuni ya mauaji, ambayo mengi ukiangalia yamekuwa yakisababishwa na migogoro ya ardhi, wivu wa mapenzi na ushirikina, tumekuja hapa kukutana na viongozi mbalimbali, lengo ni kukumbushana tunafanya nini kutokomeza matukio ya aina hii yasitokee, tumetoka na jambo la msingi kwamba turudi katika maeneo yetu, tuhakikishe yanakuwa salama kwa kutoa elimu na kuwafuatilia watu wote wanaojihusisha na mauaji” amesema kamishna wa polisi jamii Tanzania, Faustine Shilogile.

Kwa upande wake mratibu wa kitengo cha kusuruhisha migogoro na kutetea haki za binadamu kutoka Kanisa la Kiinjili la Kirutheli Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Magharibi (DKMG) Naomi Kanyonyi amesema kuwa jamii, wazee wa kimila na taasisi za kidini wamewaacha vijana waingine kwenye ndoa bila elimu yoyote ya uvumilivu, na matokeo yake wanapoingia kwenye ndoa wanafikiri wakitumia ukatili kumaliza ukatili watafaulu, kumbe wanaongeza matukio.

“Katika Wilaya sita tunazofanya nazo kazi, tumepokea migogoro 771, mingi inahusu ndoa changa za umri wa kuanzia miaka 0 hadi 5 na wanaoongoza kuleta migogoro ni wanawake ambayo ni 507, migogoro 264 imeletwa na wanaume lakini wanaume wengi wanaripoti kunyimwa unyumba, ina maana wao hawapigwi, maana kwa miaka 12 niliyofanya kazi hii ni mwanaume mmoja aliripoti kupigwa katika ndoa” amesema Kanyonyi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live