MKUU wa Mkoa wa Simiyu David Kafulika amewataka madiwani kuwatumikia wananchi kwa bidii na kuacha alama ambayo itakumbukwa hata baada ya kumaliza muda wao.
Kafulila amesema hayo katika kikao Maaalum cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri za wilaya za Maswa na Bariadi kilichojadili hoja na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu wa Serikali (cag) kuhusu hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka fedha 2019/2020.
Amesema amesema Wilaya ya Maswa ni kubwa kuliko hata baadhi ya nchi kama Rwanda na Singapore.
“Hivyo itendeeni haki Maswa, pili, Wilaya ya Maswa ni wilaya iliyofanya vizuri sana katika mapinduzi ya Viwanda, mmeonyesha mfano mzuri sana wa mapinduzi yanayopaswa kulindwa,” amesema.
Amesema viwanda hivyo vinapaswa kuwa chanzo cha mapato na sio chanzo cha matumizi na ili kulifanikisha hilo tayari Soko la Mitaji la Dar Es salaam (DSE) wamekubali kwenda Simiyu kubadilishana uzoefu na kuona ni jinsi gani na nini kifanyike ili viwanda hivi viwe endelevu.
“Mmeanzisha baadhi ya viwanda na viwanda ni biashara, hivyo ni lazima hivi viwanda viendeshwe kibiashara na kwa faida. Changamoto ninayoiona hapa ni namna ya kuviendesha viwanda hivyo kwa faida,” alisema.