Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kaburi la mbwa Nachingwea lawa kivutio

58407 Pic+kaburi

Sun, 19 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ama hakika ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni.

Kaburi la mbwa lililo umbali wa mita 500 kutoka katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Nachingwea ni kati ya maajabu yanayowafanya watalii kulitembelea baada ya kugeuka kuwa kivutio cha utalii.

Kwa kawaida wengi wamezoea kuchimba mashimo, kuzika mbwa na kufukia kiholela huku eneo la juu likikosa ishara yoyote kuonyesha kuwa mnyama alizikwa.

Tofauti na hilo, historia inaonyesha kuwa mbwa anayeitwa ‘Judy’ alizikwa na kujengewa kaburi tofauti na mbwa wengine kutokana na umahiri wake kwenye kazi ikiwamo kwenda sokoni.

Akizungumza na Mwananchi, mkuu wa wilaya hiyo, Rukia Muwango alisema mbwa huyo alikuwa anamilikiwa na Mzungu anayejulikana kwa jina la Phills kutoka Uingereza ambaye aliishi kwenye wilaya hiyo miaka ya 1950.

Alisema Mzungu huyo aliyekuwa amewekeza kwenye kilimo cha karanga alimpenda mbwa wake na kumfanya msaidizi wake.

Pia Soma

“Huyu Mzungu alimpenda sana mbwa wake ambaye alikuwa msaidizi wake wa ndani, alikuwa akimtuma sokoni, posta, buchani na mahali kwingineko,” alisema mkuu huyo wa wilaya.

Alisema kuwa mbali na kazi hizo, mbwa huyo alikuwa ndiye mlinzi wa makazi yake na rafiki yake wa karibu hivyo kuwa na thamani kubwa.

Muwango alisema siku mbwa huyo alipokufa, Mzungu huyo aliumia na kuomboleza msiba wake.

Alisema kutokana na uchungu wa kufiwa na mnyama aliyempenda aliamua kumzika kwa heshima huku akimjengea kaburi la zege na kulisakafia.

“Mwaka juzi (2017) ndugu wa Phills kutoka Ulaya walikuja ofisini kwangu wakasema wamekuja kuona kaburi la mbwa,” alisema Muwango.

Alisema kuwa kaburi hilo lilikuwa limevunjwa na kung’olewa kibao kilichokuwa kimeandikwa jina lake na watu wasiojulikana ambao walidhani wangepata utajiri wowote lakini hawakuambulia kitu.

Muwango alisema kwa sasa kaburi hilo limegeuka kuwa kivutio cha utalii kwa sababu wageni wengi wanaotembelea wilaya hiyo hupenda kwenda kulitazama.

Katika ukurasa wake wa Instagram, mkuu huyo wa wilaya ameposti historia nzima ya kaburi hilo huku wachangiaji wakisikitishwa na hatua ya watu kulivunja na kuliharibu kaburi hilo wakidhani watakuta mali.

Baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo waliotoa maoni yao kwenye ukurasa wa kiongozi huyo walisema Mzungu huyo aliamua kumzika mbwa wake kwa heshima kwa sababu anajua thamani ya wanyama.

kakati wa kukuzautalii

Muwango akielezea mkakati wa kukuza utalii wa wilaya hiyo mkuu huyo wa wilaya alisema kwa sababu Nachingwea ni kati ya wilaya zilizo na historia ya utalii wamejipanga kuhakikisha wanatangaza vivutio vyote vilivyopo.

“Kuna nyumba ambayo hayati Samora Masheli (aliyekuwa Rais wa Msumbiji) wakati akipigania uhuru alikuwa akiitumia kuongea na makamanda wake wakipanga harakati mbalimbali za kuwashinda mahasimu wao, maeneo haya yote tunayaweka kwenye muonekano mzuri ili yaendelee kuvutia,” anasisitiza Muwango.

Alisema pia kwenye wilaya hiyo kuna Mlima Ilulu ambayo umeacha historia kati ya wamwela na wangoni.

“Kwa hiyo watu wanaweza kuja kujifunza mambo mengi hapa kwetu Nachingwea,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz