Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KOICA yafufua jengo la msaada wa kisaikolojia Dar

Jengo Pic Data KOICA yafufua jengo la msaada wa kisaikolojia Dar

Mon, 15 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Taasisi ya Ustawi wa Jamii, imezindua jengo la 'Kituo cha elimu, ushauri na msaada wa kisaikolojia' lililogharimu Sh34 milioni.

Jengo hilo ambalo lilisitisha huduma zake tangu mwaka 2019 kutokana na kuchakaa, limekarabatiwa na Jumuiya ya Watanzania waliosoma Korea (KOICA).

Akizindua jengo hilo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jami, Jinsia, Wazee na Watoto- Idara Kuu Maendeleo ya Jamii, Dk John Jingu amesema huduma za msaada wa kisaikolojia ni muhimu kwa jamii yoyote ile.

Amesema kumekuwa na matukio mbalimbali ya kikatili, hivyo endapo watu hao wangepata msaada wa kisaikolojia wasingeyafanya matukio hayo.

"Unapozungumzia maendeleo yoyote kwa ustawi wa jamii huduma ya kisaikolojia ni muhimu, jamii ambayo ina mwingiliano wa mambo mengi ambayo wakati mwingine yanasababisha changamoto kwa baadhi ya watu kupata msongo wa mawazo na kufanyiana ukatili na mwingine anajitoa uhai wake.

"Hawa watu wanaofanya hivi endapo wangepata msaada wa kisaikolojia wasingeyafanya hayo. Na mimi nimekutana na wahanga wengi, baadhi ya watu wanaofanya matukio haya ukiongea nao unaona kabisa kama angepata huduma ya kisaikolojia pengine suluhisho lingekuwepo," amesema Dk Jingu.

Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Dk Joyce Nyoni amesema kukamilika kwa kazi ya kukarabati kituo hicho kutaboresha na kurahisisha mazingira ya utoaji huduma.

"Napenda nitoe shukurani zangu za dhati kwa KOICA kwa ukarabati wa kituo utakaopelekea urejeshwaji wa huduma. Mchango wao kwetu ni mkubwa sana na kwa niaba ya wafanyakazi na wanafunzi wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii nipende kuwahakikishia KOICA, jengo hili litakwenda kutumika na kuleta tija na matokeo chanya kwa jamii ya Watanzania," amesema Joyce.

Ameongeza kuwa kituo hicho kitatoa ushauri wa mahusiano ya ndoa, familia, malezi, kisaikolojia, makuzi ya watoto na vijana, uraghibu na marekebisho ya tabia, Elimu na ushauri kuhusu sheria na migogoro ya kazi, pamoja na Afya ya uzazi kwa vijana.

Chanzo: mwananchidigital