Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jokate: Changamoto ni kubadili mtazamo wa Wanakisarawe

30285 Pic+jokate Jokate Mwegelo, DC Kisarawe

Thu, 6 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kisarawe ni wilaya kongwe nchini inayoongozwa na kijana. Wakati Mkuu wa Wilaya hiyo, Jokate Mwegelo akiwa na umri wa miaka 31, wilaya yenyewe ilianzishwa mwaka 1905, sawa na umri wa Jiji la Nairobi.

Hata hivyo, maendeleo yake bado yanasuasua, jambo linalomnyima Mwegelo usingizi kama anavyoeleza katika mahojiano na mwananchi. Endelea

Swali: Kuna changamoto ya muda mrefu Kisarawe ya upatikanaji wa maji ukiwa mkuu wa wilaya mpya, una suluhisho la tatizo hili?

Jokate: Ni kweli tunayo changamoto ya upatikanaji wa maji kutokana na wilaya yetu kuwa na miamba mingi, lakini ardhi yake ina rutuba na mabonde mengi likiwamo la Mto Ruvu na chanzo CHA mto Msimbazi.

Tumepata mradi mkubwa wa ujenzi wa tangi la maji eneo la Mnarani utakaogharimu Sh10.8 milioni. Hili litakuwa na uwezo wa kubeba lita 6 milioni huku mahitaji ya wilaya yakiwa lita milioni nne kwa siku.

Kutokana na ukubwa wa tatizo, tumekubaliana na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) Kisarawe iwe eneo lao la kimkakati.

Swali: Umesema kupatikana maji kutafungua fursa nyingine, ni zipi hizo?

Jakate: Mbali na maji, wiki hii nilianza mazungumzo na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa ajili ya kuanza ujenzi wa nyumba.

Kuna fursa ya utalii itokanayo na hifadhi nne za misitu ikiwamo Pugu, Masanganya, Ruvu Kusini na Kazimzumbwi.

Tunataka kuangalia kwenye hayo maeneo na kuyaboresha kwa ajili ya utalii. Hapa hakuna hoteli, kuna nyumba za wageni mbili, hivyo miongoni mwa mikakati ya kuboresha eneo la utalii ni pamoja na kujenga hoteli.

Hii itakuwa fursa ya wageni ukizingatia ni kilomita 20 kufika uwanja wa ndege na ni rahisi kwenda Selou kupitia Kisarawe kuliko kupita Rufiji.

Swali: Katika kuboresha elimu, nini mkakati wako?

Jokate: Mikakati ipo mingi ikiwamo ule wa kambi. Tulifanya kambi ya miezi mitatu ya wanafunzi waliokuwa wanajiandaa kufanya mitihani ya kidato cha nne.

Lakini kama nilivyoanza kukueleza hapo awali, mitizamo ya wakazi wa Kisarawe bado inahitaji msukumo sana, kwa mfano kesi nyingi za mimba zinafeli kwa sababu wazazi hawatoi ushirikiano, wanachoangalia ni namna gani huyo kijana au mwanaume atahudumia familia.

Kesi nyingine nilikwenda kuifutilia juzi wazazi walikuwa wanataka wamwozeshe mwanafunzi. Kijana akakamatwa, kazi ikawa kwa binti mwenyewe, anasema anampenda huyo mwanaume na hatasoma na hata akifungwa atamsubiri atoke waendeleze maisha.

Huu ni mtizamo wa wasichana wengi ambao wazazi wanaubariki wanasema “Ameshasema hawezi kusoma bora aolewe, la sivyo atakuja kuzalia nyumbani.”

Swali: Fursa nimezisikia, lakini wakazi wana maisha ya kawaida?

Jokate: Changamoto ni mitizamo yao, bado wanahitaji msukumo hususani kwenye suala la uchumi. Kwa mfano eneo la Malui lina bonde na zao la pilipili linastawi sana, lakini wanaolima ni wazee, vijana wanataka bodaboda.

Nataka kuwawezesha vijana 5,000 watakaojikita kwenye kilimo. Nataka walime kisasa naandaa miundombinu, kwa sababu kuwapa mikopo pekee haitosi wanahitaji usimamizi zaidi.

Mbali na hilo tuna mpango wa kuomba kuwe na stesheni eneo la Visegese katika reli ya Kisasa (SGR), hii itaongeza mwingiliano wa watu ambao utasaidia kubadili mitizamo ya wazawa hususani vijana.

Chanzo: mwananchi.co.tz